Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mbeya kimesema kinaendelea kutekeleza siasa za maendeleo kwa vitendo kwa kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, huku kikieleza namna Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anavyoendelea kusukuma mbele miradi ya maendeleo nchini.
Miongoni mwa miradi hiyo ni utoaji wa Sh. Mil. 40 kupitia halmashauri ya wilaya ya Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wavulana katika shule ya sekondari Mwaselela.
Kauli hiyo ilitolewa leo Mei 22, 2026 na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM taifa (MNEC) kupitia mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, wakati akikabidhi matofali 5,000 kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo.

Mwaselela amesema utoaji wa matofali hayo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Hizi ni jitihada zinazofanywa na Rais Samia, sisi watendaji wake wa chini hatuna budi kuunga mkono……tumeona maeneo mengi miundombinu ya elimu imeboreshwa kwa kiasi kikubwa, hususan vijijini, na wananchi wameona kazi iliyofanyika,” amesema Mwaselela.
MNEC Mwaselela alitembelea shule hiyo mwezi Aprili 2026 kwa lengo la kuwapongeza walimu na wanafunzi kufuatia ufaulu mzuri wa kidato cha Nne mwaka 2025.
Katika ziara hiyo, walimu na wanafunzi waliwasilisha changamoto ya maji pamoja na upungufu wa bweni. changamoto ya maji tayari imepatiwa ufumbuzi kupitia uchimbaji wa kisima, huku ujenzi wa bweni ukiendelea baada ya kukabidhiwa matofali hayo 5,000 kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa mradi huo.

Wanafunzi, walimu na wananchi wameendelea kumpongeza Rais Samia pamoja na MNEC Mwaselela kwa juhudi zao za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuendeleza sekta ya elimu.
Mkazi wa Mbalizi, Juma Said, amesema Mwaselela amekuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya, hasa sekta ya elimu.
“Tumeshuhudia katika shule ya sekondari Nsalala kulikuwa na changamoto ya vyoo, lakini alichukua hatua na kujenga vyoo hivyo kwa gharama zake mwenyewe. Viongozi wa aina hii wanapaswa kuungwa mkono wanapofanya mambo ya maendeleo,” amesema Said.


More Stories
Itunda: Serikali yaleta mageuzi hospitalini
TMA yatoa elimu ya hali ya hewa kwa wavuvi
Twange aeleza kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi wa Mradi wa Hale