May 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CRDB Foundation,Zuchu wazindua jukwaa la “Zuchu – IMBEJU Masterclass

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na msanii wa Bongofleva, Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu wamezindua jukwaa la “Zuchu – IMBEJU Masterclass” linalolenga kuwawezesha vijana katika tasnia ya muziki na ubunifu kupitia elimu, mafunzo na fursa za kiuchumi ili kunufaika zaidi na vipaji vyao.

Ushirikiano huo unalenga kuwapa vijana elimu ya fedha, mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa chapa, ujumuishi wa kidigitali pamoja na kuwaunganisha na huduma za fedha zitakazowawezesha kukuza vipaji vyao kuwa biashara endelevu.

Kupitia ushirikiano huu, vijana wa tasnia ya ubunifu watanufaika na mafunzo kutoka kwa wataalamu wa sekta ikiwemo BASATA, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na wadau wa tasnia ya muziki na ubunifu nchini.

Jukwaa hili linatarajiwa kuongeza ajira na kukuza uchumi bunifu nchini kwa kuwawezesha vijana kutumia vipaji vyao kujenga biashara endelevu na kuongeza mchango wao katika
uchumi wa Tanzania.

Zuchu amesema anakusudia kulitumia jukwaa hili kuwapa
wasanii wachanga, ma-DJ, wanenguaji, mameneja wa wasanii na watu wengine wanaojihusisha na muziki uzoefu wake wa mambo ya kuepuka, jinsi ya kujiandaa kuwa maarufu na namna ya kusimamia fedha watakazozipata pale soko litakapowapokea.