January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya wakulima walioshiriki kwenye maonesho ya matumizi ya mashine ya kuchakata zao la dengu wakilisha dengu kwenye mashine hiyo tayari kwa kuzichakata, maonesho ambayo yamefanyika katika kijiji cha Mwongozo kata ya Mwenge wilayani Shinyanga. Picha na Suleiman Abeid

Kampuni yapongezwa kwa ubunifu mashine ya uchakati zao la dengu

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

WAKULIMA wa zao la dengu wilayani Shinyanga wameipongeza Kampuni ya Agricom Africa yenye makao yake Jijini Dar es Salaam kwa kutengeneza mashine maalumu itakayowasaidia kuchakata mazao yao na kuweza kuyaongezea ubora.

Baadhi ya wakulima walioshiriki kwenye maonesho ya matumizi ya mashine ya kuchakata zao la dengu wakilisha dengu kwenye mashine hiyo tayari kwa  kuzichakata, maonesho ambayo yamefanyika katika kijiji cha Mwongozo kata ya Mwenge wilayani Shinyanga. Picha na Suleiman Abeid

Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na wakulima wa kijiji cha Mwongozo kata ya Mwenge wilayani Shinyanga wakati wa maonesho ya matumizi ya mashine inayochakata mazao ya dengu na mpunga yaliyofanyika katika kijiji hicho.

Wakulima hao walisema kutengenezwa kwa mashine hiyo ya kisasa kutawasaidia kuongeza ubora wa zao la dengu ikilinganishwa na hapo awali walipokuwa wakichakata zao hilo kwa kusambaza chini dengu na kisha kuzikanyaga kanyaga kwa treka ili kuondoa maganda yake.

Mmoja wa wakulima hao, Kwiyolecha Nkilijiwa alisema teknolojia iliyobuniwa na Kampuni ya Agricom Africa itakuwa ni mkombozi kwa wakulima wa zao la dengu na hata wale wanaolima mpunga ambapo pia baada ya kuuvuna hutumia njia ya kupiga kwa mikono ili kuutoa kwenye mashina yake.

“Utaalamu wa uchakataji dengu kwa kutumia mashine hii utakuwa mkombozi kwetu, unafaa maana kwanza utapunguza kiasi cha dengu kinachopotea pale tunapochakata kwa kutumia trekta njia ambayo hata hivyo ina gharama kubwa ikilinganishwa na hii ya kisasa,”

“Vilevile upande wa gharama zitapungua sana, maana kwa kutumia trekta tunaingia gharama nyingi, kwanza usombe dengu kutoka shambani na kupeleka eneo la wazi kwa ajili ya kuzikanyanga na trekta, kisha uweke watu wa kuzipeta ili kuondoa takataka na mawe lakini kwa teknolojia hii kwa kweli tutapunguza gharama,” alieleza Nkilijiwa.

Naye mmoja wa wanunuzi wa zao la dengu kutoka wilayani Magu mkoani Mwanza, Anthony Charles alisema uchakataji wa dengu kwa kutumia mashine ya kisasa utawezesha kupatikana kwa dengu zenye ubora tofauti na hivi sasa ambapo hulazimika kufanya kazi ya ziada ya kuchambua takataka zinazokuwemo baada ya kuchakatwa kwa trekta.

“Nimeangalia mashine hii, kwa kweli ni nzuri, iwapo wakulima watakubali kuitumia hata sisi wanunuzi wa zao la dengu tunaamini tutapata dengu zenye ubora, maana kwa sasa tunaingia gharama mara mbili, kwanza ya kununua lakini pia kuweka watu wa kupepeta kuondoa takataka, mashine hii inapuliza uchafu wote,” alieleza Charles.

Kwa upande wake Ofisa mauzo kutoka Kampuni ya Agricom Africa, Christina Mabula alisema kampuni yao imebuni mashine hizo kwa lengo la kuwasaidia wakulima katika uchakataji wa mazao ya dengu na mpunga sambamba na kuongeza ubora wa mazao hayo.

Christina alisema mazao yanayochakatwa kwa kutumia mashine hizo za kisasa yanakuwa na ubora ikilinganishwa na yale yanayochakatwa kwa kutumia njia za asili mfano uchakataji wa zao la dengu kwa kuzikanyaga kanyaga na trekta ambapo nyingi huharibika na pia mkulima kulazimika kufanya kazi ya ziada ya upepetaji.