Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizoingizwa nchini kinyume na kisheria.
Hayo yamesemwa leo Mei 13,2026 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Amesema, ukamataji huo ni matokeo ya operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Aprili, 2026.

“Kemikali zilizokamatwa ni Cyclohexanone zenye ujazo wa lita 16,048 pamoja na Extra Neutral Alcohol (ENA) zenye ujazo wa lita 50,000,” amesema Kamisha Jenerali Lyimo.
Pia, amesema kupitia operesheni hiyo, magari mawili yaliyohusika katika usafirishaji yanashikiliwa, na watuhumiwa wawili wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo amesema, uchunguzi umebaini kuwa kemikali aina ya Cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment Company LTD bila kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kukosa vibali kutoka mamlaka husika.
Aidha, amesema kemikali aina ya Extra Neutral Alcohol (ENA) zilikuwa zikisafirishwa kwa kutumia magari ya mafuta aina ya Petrol yaliyokuwa yamebandikwa vibali vya kughushi.

Amesema, hali hiyo imetajwa kuwa ni sehemu ya mtandao wa kihalifu unaolenga kuzichepusha kemikali hizo kwa matumizi haramu.
Kamishina Jenerali Lymo amesema, kemikali aina ya Cyclohexanone hutumika kuzalisha dawa za kulevya aina ya Phencyclidine (PCP) na kwamba kiasi kilichokamatwa kingeweza kuzalisha takribani tani 11.4 za dawa hizo haramu nchini.
“Kutokana na udhibiti wa dawa za kulevya kuimarika duniani, mitandao ya kihalifu imekuwa ikitumia kemikali bashirifu kuzalisha dawa za kulevya katika maabara bubu,” amesema.
Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imesema sambamba na operesheni hiyo, ilifanya misako katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Morogoro, Dodoma.

Pia, ekari 38.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku watuhumiwa 84 wakikamatwa kuhusiana na matukio hayo.
Mamlaka hiyo imeonya kuwa itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wote watakaobainika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya pamoja na uchepushaji wa kemikali bashirifu.
Amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.


More Stories
Maisha ya machozi yageuka matumaini
CHWs waimarishwa kuwabaini watoto wenye changamoto
Wakazi Nungwi kunufaika na huduma za kidijitali