May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aga Khan Hospital yaja na suluhisho ya changamoto ya Uzito uliopitiliza

Na Mwandishi wetu,t

Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imezindua rasmi kliniki yake maalumu ya Comprehensive Obesity Clinic kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye changamoto ya uzito uliopitiliza kudhibiti hali hiyo na kuboresha afya zao kwa ujumla.

Kliniki hiyo inatoa huduma shirikishi kwa kushirikisha wataalamu kutoka fani mbalimbali, ikiwemo madaktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula, magonjwa ya moyo, magonjwa ya homoni, pamoja na wataalamu wa lishe. Lengo ni kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma jumuishi na maalumu kulingana na mahitaji yao katika kudhibiti uzito na magonjwa yanayohusiana nayo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dkt. Musolwa Ngwanasuyi, Daktari Bingwa wa Mfumo wa Chakula, amesema uzito uliopitiliza mara nyingi huhusishwa na matatizo ya kimetaboli kama mafuta kwenye ini.

“Mara nyingi hali hii huathiriwa na sababu za kimetaboli na mnenge’enyo wa chakula. Hivyo, tathmini ya kina ya kitabibu ni muhimu ili kubaini njia bora zaidi ya matibabu kwa kila mgonjwa,” amesema Dkt. Ngwanasuyi.

Dkt. Nadeem Kassam, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, amebainisha kuwa uzito uliopitiliza huongeza hatari ya kupata shinikizo la damu, ugonjwa wa mishipa ya moyo moyo kushindwa kufanya na kiharusi.

“Unene mara nyingi husababisha matatizo ya moyo yanayoanza mapema na kupunguza ufanisi wa moyo kwa muda. Uchunguzi wa mara kwa mara na mabadiliko ya mtindo wa maisha ni muhimu katika kuzuia madhara ya muda mrefu kwa moyo na kuboresha afya ya wagonjwa,” amesema.

Kwa upande wake, Dkt. Hanifa Mbathe, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Homoni, amesema uzito uliopitiliza unahusiana kwa kina na hitilafu za homoni mwilini na michakato ya kimetaboli.

“Sababu hizi za ndani ndizo huamua jinsi mwili unavyohifadhi mafuta, kudhibiti hamu ya kula na mvitiko wake kwa mabadiliko ya mtindo wa maisha. Hivyo, suluhisho bora linahitaji zaidi uchunguzi wa matibabu ya kibingwa ili kujua na kushughulikia chanzo cha tatizo hilo,” amesema Dkt. Mbathe.

Kliniki hiyo inakuja wakati uzito uliopitiliza ukiwa changamoto inayoongezeka duniani na hapa nchini, mara nyingi ikiambatana na magonjwa kama kisukari, magonjwa ya moyo, na matatizo ya kupumua wakati wa usingizi