May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yahimiza mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imehimiza mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuendana na hali halisi ya siasa za Ulimwengu ya sasa, huku ikisisitiza kuwa itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha chombo hicho kinakuwa na uwakilishi mpana, uwazi, na uwajibikaji zaidi kwa mataifa yote.

Hayo yameelezwa Mei 11, 2026 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki Mhe. James Millya, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kuhusu Mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa “Africa Forward Summit” unaondelea Jijini Nairobi, Kenya .

Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Kenya Mhe. Musalia Mudavadi.

Aidha,Millya amekumbushia msisitizo uliotolewa na Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Philip Mpango, wakati wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa dunia imebadilika sana katika miongo minane iliyopita tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa hivyo ni lazima kukubali mageuzi yanayoakisi karne ya 21.

Hoja kuu iliyowasilishwa katika Majadiliano hayo ni Afrika kutowakilishwa ipasavyo katika Baraza la Usalama, licha ya kuwa na zaidi ya robo ya wanachama wote wa Umoja wa Mataifa na kuwa kitovu cha masuala mengi yanayojadiliwa.

Imebainishwa kuwa mjadala huo wa mageuzi haupaswi kuishia kwenye Baraza la Usalama pekee, bali uendelee hadi kwenye taasisi nyingine za Fedha za Kimataifa, kama Benki Kuu ya Dunia na IMF.