

Na Mwandishi wetu,WHUSM
MAAFISA Habari wa Serikali wametakiwa kuongeza ufanisi katika kutangaza shughuli za Serikali huku wakizingatia mabadiliko ya teknolojia.
Msisitizo huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka wakati akifunga Kikao Kazi za 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki, na Uhusiano Serikalini.
.Mtaka amewaeleza maafisa hao kuendelea kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi kwa kuwapatia taaarifa sahihi zinazolenga kubadilisha maisha ya wananchi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu pamoja na fursa zilizopo katika sekta ya burudani.
“Mnapohudhuria vikao kazi hivi tafuteni pia fursa ambazo zitabadilisha maisha yenu binafsi nje ya kazi, tafuteni uwekezaji katika biashara, kilimo na sehemu nyingine ili kuwa na maisha bora zaidi baada ya kustaafu”, ameseisitiza Mhe. Mtaka.
Awali Kaimu Mkurugenzi Idara ya Habari -MAELEZO aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Kelvin Kanje akimkaribisha Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa, Kikao Kazi hicho kimekuwa na mafanikio kwa kuwa maafisa wamepata elimu na mafunzo mbalimbali yanayolenga kuongeza ufanisi katika majukumu yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Eleuteri Mangi, amesema kikao kazi hicho kimekuwa chachu ya maafisa kujipima utendaji kazi wao na chachu ya kufanya vizuri katika taasisi zao, akisisitiza vikao hivyo kuendelea kufanyika.
Naye Afisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Pettu Ogilo amesema kikao kazi hicho kimekuwa na manufaa kwake kwani masuala mengi wanayoelekezwa yanamsaidia katika utekekezaji wa majukumu yake, pia amepata elimu pamoja na kubadilishana uzoefu na maafisa wenzie.

More Stories
Maisha ya machozi yageuka matumaini
DCEA yakamata kemikali bashirifu lita 66,048
CHWs waimarishwa kuwabaini watoto wenye changamoto