Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo amesema, Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, akisisitiza kuwa lugha hiyo sasa imepata mafanikio makubwa kimataifa.
Akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo Vungeni Jijini Dodoma kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 leo Mei 4,2026 , Waziri amesema kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Tanzania imeongoza juhudi za kuhamasisha matumizi ya Kiswahili, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa lugha hiyo kukubalika kuwa lugha rasmi ya Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Amesema hatua hiyo ya kihistoria ilifikiwa wakati wa Mkutano Mkuu wa 43 wa UNESCO uliofanyika Samarkand, Uzbekistan kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 13, 2025, na kuifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kupata hadhi hiyo.
“Kwa mafanikio haya, Kiswahili sasa ni lugha rasmi katika Jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika, Umoja wa Wazalishaji Almasi Afrika pamoja na UNESCO,” amesema Waziri.
Aidha, Waziri amebainisha kuwa Kiswahili kinaendelea kupata heshima ya kipekee duniani, kikiwa lugha pekee ya Afrika yenye siku maalum ya kuadhimishwa Julai 7 ya kila mwaka .
Katika kuimarisha matumizi ya Kiswahili kwenye teknolojia za kisasa, Waziri Makonda amesema Wizara kupitia Baraza la Kiswahili Tanzania ( BAKITA ) imefanya mazungumzo na UNESCO pamoja na wadau wa maudhui ya mtandaoni ili kupanua matumizi ya Kiswahili katika mitandao mikubwa ya kijamii kama META, TikTok na Google.
Amesema ,lengo la hatua hiyo ni kuongeza ajira na kipato kwa vijana wanaojihusisha na uandaaji wa maudhui mtandaoni.
Akisisitiza umuhimu wa lugha hiyo katika kuhifadhi utamaduni, Waziri alinukuu mithali isemayo, “Asiyefahamu lugha, hafahamu mila,” akibainisha kuwa wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya Kiswahili fasaha na sanifu.
Katika utekelezaji wa hilo, jumla ya vipindi 1,057 vimeandaliwa na kurushwa kupitia redio na televisheni mbalimbali nchini. Pia, mafunzo ya matumizi bora ya Kiswahili yametolewa kwa Waandishi Waendesha Ofisi 844, makatibu wa kamati za halmashauri 12 pamoja na wahudumu wa mapokezi na huduma kwa wateja 52.
Waziri amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika kukuza Kiswahili ili kiwe chombo madhubuti cha mawasiliano, utamaduni na uchumi wa Taifa pamoja na Afrika kwa ujumla.

More Stories
Waandishi 3,357 wapata Ithibati kupitia mfumo maalum
Samia atoa bil 20,waandaji maudhui wanufaika
Waumini wahimizwa kutumia talanta kwa uaminifu