May 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilindi yatenga fedha kukamilisha miradi viporo

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOline,Kilindi

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga John Mgalula amesema halmashauri hiyo imepanga kukamilisha miradi viporo kabla ya kuanzisha mipya, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 kupitia mapato ya ndani wametoa sh. milioni 257 kwa ajili ya umaliziaji wa miradi.

Kati ya fedha hizo, sh. milioni 105 ni umaliziaji miradi ya afya, sh. milioni 25 ni kwa ajili ya umaliziaji wa chumba cha darasa Shule ya Sekondari Kibirashi, na chumba kimoja cha TEHAMA Shule ya Kata Mabalanga. Pia sh. milioni 125 kwa ajili ya umaliziaji wa miradi ya elimu msingi shule za Ndwati, Ngeze na Lusimbi.

“Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, John Mgalula akijibu maswali ya madiwani ya papo kwa hapo.”

Amesema hayo Aprili 29, 2026 wakati anajibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa madiwani kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, na kuongeza kuwa halmashauri imeendelea kupokea fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi mbalimbali katika sekta za elimu na afya ili iweze kutoa huduma kwa wananchi.

“Wilaya ya Kilindi ina jumla ya miradi viporo 180, kati ya miradi hiyo, Sekta ya Afya ina miradi 13 (zahanati saba na vituo vya afya sita), elimu sekondari miradi 57 (maabara 39, madarasa 15, maktaba moja na majengo ya utawala mawili), na elimu ya msingi miradi 110 (madarasa 100 na nyumba za walimu 10)

“Wilaya ya Kilindi imeendelea kuweka kipaumbele kwenye ukamilishaji miradi viporo katika sekta zote, ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kupitia mapato ya ndani imetoa sh. milioni 257. Kati ya fedha hizo, sh. milioni 105 ni umaliziaji miradi ya afya, sh. milioni 25 ni kwa ajili ya umaliziaji wa chumba cha darasa Shule ya Sekondari Kibirashi, na chumba kimoja cha TEHAMA Shule ya Kata Mabalanga. Pia sh. milioni 125 kwa ajili ya umaliziaji wa miradi ya elimu msingi shule za Ndwati, Ngeze na Lusimbi”amesema Mgalula.

Mgalula amesema halmashauri hiyo ina mikakati ya dhati ya kuhakikisha inakarabati shule kongwe wilayani humo. Mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kutenga fedha kupitia mapato ya ndani, kuomba fedha kutoka Serikali Kuu, wahisani na kuandika maandiko ya kuomba fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

“Mpango wa ukarabati wa shule hizi ni endelevu. Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 halmashauri ilipokea sh. milioni 101 kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Msingi Ludewa na sh. milioni 101 kwa ajili ya ukarabati Shule ya Msingi Sangeni. Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri imepokea sh. 581,215,110 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe”amesema Mgalula.

Mgalula alikuwa anajibu maswali ya Diwani wa Kata ya Kimbe, Yahaya Calamba kutaka kujua halmashauri ina mpango gani wa kuhakikisha miradi viporo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi inakamilika na kuweza kutoa huduma kwa wananchi.

Calamba ambaye kwa taaluma ni mwalimu, pia alitaka kujua, halmashauri ina mpango gani wa kufanyia ukarabati shule kongwe hasa zilizopo Kata ya Songe ambayo ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Kilindi.

“Diwani wa Kata ya Kimbe, Yahaya Calamba akiuliza swali la nyongeza.”
“Madiwani wakiwa kwenye Baraza.”
“Wakuu wa Vyombo vya Usalama, Wakuu wa Idara na Vitengo, Afisa Tarafa na waalikwa wakiwa kwenye Baraza.”