
Na Israel Mwaisaka, Nkasi
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imeanza utekelezaji wa mradi wa Huduma Endelevu za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (SRWSSP), utakaotekelezwa katika vijiji 16 kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja s kuimarisha hali ya usafi wa mazingira.
Mradi huo unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali ambayo imekuwa ikiathiri shughuli za kiuchumi na kijamii pamoja na ustawi wa afya zao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Dkt. Benjamin Chota, amesema utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa mfumo wa malipo kulingana na matokeo (Results-Based Financing).
Ameongeza kuwa viashiria vya mradi huo vitahusisha hali ya usafi katika vituo vya kutolea huduma za afya, shule pamoja na kaya za wananchi, hatua ambayo inalenga kuhakikisha mradi hauishii tu kwenye upatikanaji wa maji bali pia unachangia kuboresha afya ya jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijualikali, amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinapata maji ya uhakika na kwamba mradi huo utahusisha uunganishaji wa mifumo ya maji kwenye majengo ya vituo vya afya, hali itakayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha alitumia fursa kuwataka wakandarasi kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati na wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo mapema.
Utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu katika jitihada za serikali za kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma bora za maji safi na usafi wa mazingira, jambo litakalosaidia kupunguza magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.

More Stories
Serikali yaimarisha hatua za kudhibiti bei za Mafuta
Kamati kuu CCM yampitisha Mtafikolo kugombea ubunge Isimani
Mtoto afariki kwa kusombwa na maji akivuka mto