Na Mwandishi wetu,Timesmajira
MKUU wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema Muungano sio majengo bali ni umoja wa Watanzania wote.
Shaka amesema hayo juzi mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Suleiman Abdulla wakati wa uzinduzi wa majengo ya Chuo Cha Ualimu Dawaka, kilichopo wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Amesema tarehe 26 Aprili 1964, waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Sheikh Aman Abeid Karume walifanya uamuzi wa kihistoria wa kuunganisha Tanganyika na Zanzibar kuwa Tanzania moja.
“Leo, miaka 62 baadaye, Muungano umesimama, umesimama kwa amani, umesimama kwa udugu na umesimama kwa maendeleo,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya, ameongeza kuwa muungano si majengo, muungano si karatasi bali ni sisi na ni umoja wetu wa kila siku.

Amesema chini ya umoja huo, Tanzania imepata amani ya kudumu, imepata sauti moja Afrika na Duniani.
Amesema chini ya Muungano tumepata nguvu ya pamoja katika kujiletea maendeleo, hivyo tuulinde Muungano huo.
“Muungano huu tuuenzi kwa vitendo kwa kufanya kazi, kupendana na kuvumiliana. Muungano wetu umetupa amani. Umetupa utambulisho. Umetupa nguvu ni wajibu wetu sote kuulinda, kuuenzi, na kuuendeleza kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo,” amesema Shaka.


More Stories
Bodi ya REA yaridhishwa miradi mwambao ziwa nyasa
Tanzania yajinadi kimataifa katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
Exim yafanya mazungumzo na wizara ya elimu kufadhili Wanafunzi elimu ya juu