April 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake Watwishwa zigo la kusimamia maadili katika jamii

Na Israel Mwaisaka, Rukwa

‎Mkuu wa Wilaya Nkasi mkoani Rukwa Peter lijualikali amewataka Wanawake kutumia uwezo wao kujenga maadili katika jamii kwani wao ndiyo wenye jukumu la kulea familia na kuwa hilo litawezekana kama pia watakua na nguvu za kiuchumi.

‎Ameyasema hayo leo Jumapili Aprili 26,2026 kwenye kongamano la Wanawake wa Kiislamu mkoa Rukwa (JUWAKITA) lililofanyika katika msikiti Mkuu wa Ijumaa Namanyere, Nkasi ambapo alidai kuwa hivi Sasa jamii imekumbwa na tatizo la mmomonyoko wa maadili na kuwa Wanawake wanao uwezo wa kuirudisha jamii kwenye misingi inayokubalika.

‎Sheikh Mkuu wa mkoa Rukwa Rashid Akilimali kwa upande  wake alisema kuwaWanawake wa Kiislamu wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba familia zinazotawi na hilo litawezekana kama wao watajituma katika shughuli za uzalishaji mali na biashara na kuondokana na mawazo ya kuwategemea Wanaume pekee.

‎Pia aliwasihi Wanawake kuendelea kuvaa mavazi yenye staha kwani kufanya hivyo ni kujiheshimu na Kutoa utukufu mbele ya Mwenyezi Mungu huku akimuomba Mkuu wa Wilaya kuhakikisha katika ofisi za Serikali Watumishi wa Umma wanavaa nguo zenye staha wawapo kazini ili wapate uhalali wa Kutoa huduma kwa jamii .

‎Mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya kwenye kongamano hilo Fortunatusi Kaguo alidai kuwa halmashauri kupitia Ile mikopo ya asilimia 10 moja ya wanufaika ni Wanawake hivyo jumuia hiyo ya Juwakita inaweza kufuata kanuni za mikopo hiyo ili na wao wakanufaika kwa kupata mikopo isiyo na riba kwa kupata mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi.

‎Amesema kuwa wao kama Serikali jukumu lao ni kuwajengea mazingira mazuri ya kiuchumi Wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo Wanawake hivyo ni jukumu lao kama jumuia ya Wanawake wa kiislamu kutengeneza mazingira ya kukopesheka na kuweza kuanzisha miradi itakayowakwamua kwenye lindi la umasikini.

‎JUWAKITA kwa upande wao kupitia risala Yao  walidai kuwa wameanzisha shughuli mbalimbali ikiwemo ya ushonaji ikiwa ni pamoja na kutengeneza darasa la kuwafundisha Wasichana wadogo shughuli za ushonaji ili waweze kuwa na ujuzi wa kazi hiyo hiyo itakayowasaidia katika maisha Yao.

‎Wamesema kuwa licha ya mafanikio machache waliyoyapata lakini bado wanayo changamoto ya mtaji hafifu ikiwa ni pamoja na kufanyia shughuli zao kwenye nyumba za kupanga na kuwa kwa Sasa wamefanikiwa kununua kiwanja ili waweze kujenga ofisi Yao na kuwa ili kufanikiwa mpango huo wanahitaji Tshs,Mil.20.

‎Mkuu wa Wilaya kwa upande wake amewachangia Tshs,Mil,2 Wanawake hao kama sehemu ya kuunga mkono jitihada zao walizozianzisha.