April 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katimba:Msingi wa Dira 2050 ni Utawala Bora,sheria imara

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba, amesema kuwa msingi mkuu wa kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni uwepo wa utawala bora unaojengwa juu ya amani, usalama na utulivu, akisisitiza kuwa nguzo hizo ndizo zitakazobeba mustakabali wa Tanzania ya kesho.

Akijibu hoja za wabungeleo April 24,2026 bungeni jijini Dodoma wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Katimba alisema kuwa msingi huo ndiyo unaotofautisha taifa linalokua kwa bahati na lile linalojengwa kwa makusudi.

“Ni muhimu kutambua kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, sekta ya sheria imewekwa katikati ya mjadala wa uchumi wa Taifa,hii ni hatua ya kihistoria,” alisema Katimba

Alieleza kuwa mabadiliko hayo yanaonesha namna ambavyo serikali imeondoka katika mtazamo wa kuitazama sekta ya sheria kama mtumiaji wa rasilimali pekee, na sasa inaijenga kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi, mlinzi wa uwekezaji pamoja na nguzo muhimu ya kudumisha utulivu wa Taifa.

Katimba alisisitiza kuwa hakuna uchumi wa kisasa unaoweza kustawi bila uwepo wa uhakika wa sheria, huku akibainisha kuwa hakuna mwekezaji anayeweza kuwekeza bila ulinzi wa haki zake.

“Vilevile, hakuna maendeleo endelevu yanayoweza kupatikana bila mifumo ya haki inayofanya kazi kwa ufanisi, usawa na uwazi,” aliongeza.

Akifafanua zaidi kuhusu Dira ya Taifa ya 2050, Katimba alisema dira hiyo imejengwa katika nguzo tatu kuu ambazo ni uchumi imara na shindani, maendeleo ya watu na jamii, pamoja na uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, alibainisha kuwa nguzo hizo haziwezi kufikiwa bila kuwepo kwa msingi thabiti wa amani, usalama na utulivu, ambao pia unahitaji mageuzi ya kina ya kimfumo ndani ya sekta ya sheria.

“Ni lazima tujenge taifa ambalo sheria si kikwazo, bali ni daraja la maendeleo,” alisisitiza.

Aidha, aliwahakikishia wabunge kuwa wizara itaendelea kuboresha mifumo ya haki ili kuhakikisha inakuwa jumuishi, yenye ufanisi na inayoendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa.

Kauli hiyo imekuja wakati serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa mageuzi ya sekta ya sheria kama sehemu ya mkakati mpana wa kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini