Na Mwandishi Maalum,TimesMajira Online. Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein ameipongeza Kamati ya Madawati kwa shule za Serikali kwa kusimamia na kuhamasisha wahisani na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi katika kuchangia utatuzi wa uhaba wa madawati.
Ameyasema hayo juzi Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na baadae kukabidhiwa ripoti na Kamati ya Madawati ya Zanzibar ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman.
Katika pongezi zake hizo, Rais Dkt.Shein alieleza kuwa, kazi kubwa imefanywa na kamati hiyo na hatimae mafanikio makubwa yameweza kupatikana kwa asilimia 70 ya kupunguza uhaba wa madawati kwa shule za Unguja na Pemba.
Rais Dkt.Shein ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba na ile ijayo itaendelea kuiitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa madawati ili kuhakikisha wanafunzi wote wa msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba hakuna anayekaa chini.
Aidha, Rais Dkt.Shein amesema kamati hiyo aliyoiunda mnamo tarehe 27 Julai mwaka 2016 imeweza kufanya kazi nzuri ya kusimamia na kuhamasisha wahisani na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi katika kuchangia utatuzi wa uhaba wa madawati kwa skuli za Zanzibar.
Ameongeza kuwa, kamati hiyo yenye wajumbe 13 wakiongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman na Makamu Mwenyekiti wake, Riziki Pembe Juma imefanya kazi kubwa na kuna kila sababu ya kupongezwa.
Amesema kila Mjumbe katika kamati hiyo ana sifa zake hali ambayo imepelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa hatua ambayo imetokana na nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi