September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yazindua kituo cha michezo kuandaa wataalamu

Na Eleuteri Mangi,TimesMajira Online. WHUSM

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas, amezindua kituo cha michezo ili kuwaandaa na kuongeza idadi ya wataalamu wa michezo nchini.

Kituo hicho kinachoendeshwa na cha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kipo jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo, Dkt. Abbasi amesema kati ya mambo ambayo alikuwa anajifunza baada ya kukabidhiwa wizara hiyo, ilikuwa ni pamoja na uendeshaji wa shughuli za wizara na taasisi zake, hatua iliyomfanya kuagiza chuo hicho kiboreshwe ili iwe fursa ya kutengeneza wataalamu wa michezo wengi nchini.

“Tumefanya uamuzi mgumu na muhimu sana wa kuleta kituo cha chuo chetu cha michezo Malya hapa Dar es Salaam, ili kutoa na kuendeleza elimu ya michezo katika kada zote nchini na tunaamini mahitaji ni mengi sana,” amesema.

Dkt. Abbasi amesema, wameanzisha kituo ambacho kitatoa programu mbalimbali za michezo ili kuendana na hali halisi ya sekta ya michezo na kuwafanya wataalamu wa michezo, wakiwemo wachambuzi, walimu wa michezo na waamuzi kuwa na uwanja mpana katika michezo hatua inayosaidia kuendana na hali halisi ya michezo kwa mujibu wa Shirikisho la Michezo Shirikisho la Michezo Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).