Uongozi waridhishwa na mwenendo, majeruhi kikwazo; waahidi makubwa.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
UONGOZI wa Yanga SC umemrejesha kundini kocha Abdihamid Moalin, ambaye sasa atahudumu kama kocha msaidizi wa kocha mkuu Pedro Goncalves, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha benchi la ufundi la timu hiyo.
Uamuzi huo ulifikiwa Machi 23, 2026, katika kikao cha tathmini kilichofanyika makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani, jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea ripoti kutoka kwa benchi la ufundi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mara baada ya kikao hicho, uongozi wa Yanga ulibaini changamoto kuu mbili zinazoikabili timu kwa sasa, ambazo ni msongamano wa ratiba ya mechi pamoja na wimbi la majeraha ya wachezaji.
Pia ilielezwa kuwa timu ililazimika kucheza michezo saba ndani ya siku 21, hali iliyochangia kupungua kwa makali ya kikosi.
Aidha, jumla ya wachezaji wanane wanakabiliwa na majeraha tofauti, hali inayodhoofisha kikosi hicho licha ya kufanya vizuri katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.

Katika tathmini hiyo, Yanga imeonekana kuwa na mwenendo mzuri uwanjani baada ya kucheza michezo 16, kushinda 11 na kutoka sare tano bila kupoteza mchezo hata mmoja.
Timu hiyo pia imefunga mabao 32 na kuruhusu mabao matatu pekee, ikiwa na rekodi bora ya ushambuliaji na ulinzi.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, uongozi umebaini kuwepo kwa changamoto ya kiufundi, hususan katika utekelezaji wa mfumo wa uchezaji (style of play), hali inayosababisha kukosekana kwa muunganiko mzuri wa wachezaji katika baadhi ya michezo.
Kutokana na hali hiyo, klabu imeamua kumuongeza Moalin kwenye benchi la ufundi ili kusaidia kurekebisha changamoto hizo.
Kocha huyo anarejea akiwa na uzoefu mkubwa ndani ya klabu hiyo, baada ya kuwahi kushiriki katika mafanikio ya kutwaa mataji mbalimbali ya ndani.
Wachezaji wanaokabiliwa na majeraha ni pamoja na Khomein Aboubakar, Clement Mzize, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Chadrack Boka, Edmund John, Prince Dube na Laurindo Maria, huku baadhi yao wakitarajiwa kukosekana hadi mwishoni mwa msimu.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umewahakikishia wanachama na mashabiki wake kuwa timu itarejea ikiwa imara zaidi katika mzunguko wa pili wa ligi, ikiwa na dhamira ya kutimiza malengo ya msimu wa 2025/26, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC pamoja na Kombe la Shirikisho la CRDB Bank.

More Stories
Wizara,TPSF kuongeza ushiriki kongamano la kiswahili
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewaÂ
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini