Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Askari mgambo watatu jijini Mwanza,wanashikiliwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi,kwa tuhuma za mauaji ya Rashid Nyandonga(31),fundi simu na mkazi wa jeshini wilayani Nyamagana mkoani hapa.
Akizungumza Machi 22,2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,amesema,Machi 20,2026 usiku,jeshi hilo liliwakamata watuhumiwa hao na kinaendelea kuwahoji.
Mutafungwa,amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Zongoli Makongoro( 38) kazi yake ni askari mgambo
anayefanya kazi katika Kata ya Mahina na mkazi wa Bugarika wilaya
ya Nyamagana.
Genge Mwita(45),kazi yake ni mgambo anayefaya kazi katika Kata ya Igogo na mkazi wa mtaa wa Kambarage wilaya ya
Nyamagana na watatu ni Ibrahim Mwita (25) kazi yake ni askari mgambo katika
Kata ya Pamba na mkazi wa Bugando Mission wilayani Nyamagana.
Amesema,tukio hilo la mauaji lilitokea Machi 20,2026 majira ya 12:45 jioni huko
mtaa wa Mission,eneo la Sahara, Kata ya Pamba, wilayani Nyamagana.
Ambapo inadaiwa kuwa jioni hiyo ya tukio hilo askari mgambo hao
wakiwa katika mtaa huo walimtilia shaka Nyandonga ambaye kwa sasa ni marehemu kuwa anauza dawa za kulevya aina ya mirungi na kuanza kumfuatilia, ndipo mtu huyo alikimbia mbio kukwepa kukamatwa.
Kwa mujibu wa Mutafungwa,askari
mgambo hao walimfukuza na kufanikiwa kumkamata akiwa na mirungi gramu 50 ingawa mtu huyo alikuwa akihema kwa nguvu na kuonesha dalili za kuishiwa nguvu.
Askari mgambo hao ambao ni watuhumiwa kwa sasa walimpeleka Nyandonga (marehemu) hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure kwa huduma zaidi na wakati matibabu yakiendelea hospitalini hapo alifariki dunia.
Kutokana na hali hiyo jeshi la polisi mara moja liliwakamata askari mgambo hao wote watatu kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
“Askari mgambo hao wakati wakifanya ukamataji kwa mtuhumiwa huyo kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya walikuwa peke yao, na wakati huo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza halikuwa na operesheni yoyote ya ukamataji wa makosa iliyowashirikisha askari mgambo katika eneo hilo,”amesema Mutafungwa.
Hata hivyo amesema,mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi (post mortem),Machi 21,2026 katika hospitali ya Sekou-Toure ili kubaini chanzo cha kifo hicho. Ndugu wa marehemu wameshiriki katika uchunguzi huo kwa mujibu wa taratibu na umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya utaratibu wa mazishi.
Sanjari na hayo amesema,jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusiana na na endapo ushahidi utaonesha kuwa watuhumiwa hao wamehusika na mauaji hayo watawajibishwa kwa mujibu wa sharia.
Huku akitoa wito kwa askari mgambo wanapofanya ukamataji wazingatie ukamataji salama na wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kufichua uhalifu na wahalifu.

More Stories
Silinde azindua baraza la sita la Wafanyakazi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini