Na Martha Fatael, TimesMajira Online
WAKATI mjadala ukiendelea katika mkutano wa wadau wa Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (MISA TAN) 2026, tasnia ya habari imeanza kuonyesha mwelekeo mpya unaochanganya changamoto na matumaini kwa wanahabari nchini.
Akifungua mkutano huo mkoani Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya taifa.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye uelewa sahihi……lakini ni muhimu kuhakikisha uhuru wa habari unaenda sambamba na uwajibikaji,” amesema James.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa habari ili kuboresha mazingira ya kazi kwa wanahabari, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema mkutano huo umebeba dhamira ya kuimarisha tasnia ya habari inayoweza kujitegemea na kuwajibika.
“Bado tunakabiliwa na changamoto nyingi usalama wa wanahabari, uhuru wa vyombo vya habari na hata ustawi wa kiuchumi wa waandishi wenyewe,” amesema Soko.

Amesema ni wakati wa wadau kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuhakikisha tasnia hiyo inalindwa na kupewa nafasi stahiki katika maendeleo ya nchi.
Katika mijadala ya ndani ya mkutano huo, wanahabari wameeleza kwa uwazi changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo uhaba wa rasilimali, shinikizo la kazi na wakati mwingine kukosa ulinzi wanapotekeleza majukumu yao.
Mmoja wa washiriki Lucy Ulomi, amesema,wakati mwingine wanahabari hulazimika kufanya kazi katika mazingira magumu bila kuwa na vifaa vya kutosha, hali inayowalazimu kutumia juhudi binafsi ili kukamilisha majukumu yao.

Amesema pamoja na changamoto hizo, bado jamii inaendelea kutegemea kupata taarifa sahihi na za kuaminika kutoka kwao, jambo linalowaongezea wajibu mkubwa katika utekelezaji wa kazi zao.
Aidha, wadau wamejadili nafasi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa habari, wakihimiza wanahabari kutumia majukwaa ya kidijitali kwa ubunifu zaidi ili kufikia hadhira pana.

Kwa mujibu wa waandaji, mkutano huo ni zaidi ya jukwaa la majadiliano, bali ni nafasi ya kujenga mshikamano na kuimarisha sauti ya pamoja ya wanahabari nchini.
Kadri mkutano wa MISA TAN 2026 unavyoendelea, matumaini yameonekana kuwa kupitia maazimio yatakayofikiwa, tasnia ya habari itaweza kuimarika zaidi na kuendelea kulinda maslahi ya jamii kwa weledi na uwajibikaji.


More Stories
Bechina atoa futari kwa wananchi 750 Ilala
Miaka 50 ya tantrade yaimarisha biashara ya kimataifa
HaloPesa yaigusa jamii kupitia huduma yake