March 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka 50 ya tantrade yaimarisha biashara ya kimataifa

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imetoa mwaliko wa dhati kwa wadau wa biashara, wawekezaji, wazalishaji na wananchi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya TanTrade.

Imesema maadhimisho hayo ni fursa ya kipekee ya kuonesha bidhaa na huduma za Tanzania katika soko la kimataifa, kujenga mitandao ya kibiashara, kupata masoko mapya na kushirikiana katika kukuza uchumi wa taifa.Kwa mujibu wa TanTrade, miaka 50 ya taasisi hiyo ni ushuhuda wa safari ya mafanikio na ya kujivunia katika kujenga taifa lenye uchumi imara na heshima ya kimataifa.

Wakati wa maadhimisho hayo, mamlaka hiyo imetambua mchango wa viongozi waliopita, wadau wa biashara pamoja na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Imeeleza kuwa maadhimisho hayo si tu kielelezo cha ukuaji wa sekta ya biashara, bali pia ni alama ya mshikamano wa kitaifa na dira ya maendeleo inayolenga kuimarisha uchumi wa Tanzania na nafasi yake katika jumuiya za kikanda na kimataifa.

TanTrade imeendelea kusisitiza nafasi yake kama nguzo muhimu ya kukuza na kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi, kwa kutoa jukwaa linalowaunganisha wazalishaji na masoko ya kimataifa.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasiliano cha mamlaka hiyo, imeelezwa kuwa kwa kipindi cha miaka 50, TanTrade imekuwa daraja muhimu la kuunganisha wazalishaji wa ndani na masoko ya nje.

Kupitia maonesho ya biashara, misafara ya kibiashara na kampeni mbalimbali za kitaifa, imefanikisha upatikanaji wa masoko mapya na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania.Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyotajwa ni pamoja na Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, ambayo kwa zaidi ya miaka 50 yamekuwa chachu ya kukuza biashara nchini.

Mafanikio mengine ni pamoja na upanuzi wa masoko ya bidhaa, ubunifu wa kidijitali, pamoja na kuimarisha utambulisho wa taifa kupitia kampeni ya “Made in Tanzania”.Imeelezwa kuwa kampeni hiyo imeongeza thamani na heshima ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi, huku ikiimarisha uzalendo kwa wananchi kununua bidhaa za ndani. Pia imewapa wazalishaji fursa ya kujivunia kazi zao na kujiamini katika ushindani wa kimataifa.

“Kupitia kampeni hii, bidhaa za Tanzania zimepata utambulisho wa kipekee unaoonyesha ubora, ubunifu na asili ya taifa letu, hivyo kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza uchumi wa ndani,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, TanTrade imesisitiza kuwa imekuwa daraja muhimu la kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa, hatua iliyosaidia kuimarisha nafasi ya nchi katika jumuiya mbalimbali za biashara.

Kupitia ushirikiano huo, Tanzania imefanikiwa kushiriki kikamilifu katika masoko ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika, Asia na Ulaya, hali iliyoongeza fursa za biashara na uwekezaji. Ushirikiano huo umeimarisha biashara ya mipakani pamoja na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI).TanTrade pia imetoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya biashara na uwekezaji kupitia sera za uwazi na diplomasia ya uchumi.

Imeeleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, mazingira ya biashara yameendelea kuwa rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara, huku serikali ya awamu ya sita ikiendelea kuwezesha kampuni za Tanzania kushiriki katika masoko ya kimataifa na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.“Rais Samia ameonesha dira ya maendeleo inayolenga kuimarisha sekta binafsi na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje,” imehitimisha taarifa hiyo.