September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ngara wasisitizwa kutunza miradi na kijamii

Veronica Simba,TimesMajira Online. Ngara

SERIKALI imewataka wananchi wa Ngara mkoani Kagera, kutunza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii inayoendelea kutekelezwa wilayani hapa kupitia mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera (megawati 80).

Wito huo umetolewa juzi na timu ya serikali kutoka Tanzania inayosimamia mradi huo, ikihusisha Wakurugenzi wa Bodi na Kamati ya Ufundi wakiwa katika ziara ya kazi yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya kijamii, inayotekelezwa kupitia mradi husika.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na Maofisa Watendaji pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali kulipo na miradi hiyo kiongozi wa timu hiyo, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Mjumbe wa Bodi wa Kamati husika amesema endapo miundombinu hiyo ya miradi husika isipotunzwa, itakuwa ni hasara kwa serikali na wananchi walengwa.

“Miradi hii inayohusisha shule, vituo vya afya, miradi ya maji, miundombinu ya kilimo na ufugaji bora inalenga kuwanufaisha wananchi hivyo ili lengo hilo litimie, inabidi itunzwe,” amesema.