March 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Diwani Bhojani atoa nguo kwa watoto Ilala


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Diwani wa Kata ya Kisutu, Tousif Bhojani, ametoa msaada wa nguo kwa watoto wa mahitaji maalum katika baadhi ya kata za wilaya ya Ilala, ili kuwawezesha kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr kama watoto wengine katika jamii.

Msaada huo umekabidhiwa katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, ambapo madiwani wa kata tano wamepokea nguo hizo kwa ajili ya kuzigawa kwenye vituo vya watoto wenye mahitaji maalum katika maeneo yao.

Kata zilizopokea msaada huo ni Vingunguti, Buguruni, Zingiziwa, Msongola na Bonyokwa. Mgeni rasmi katika hafla hiyo ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde.

Akikabidhi msaada huo, Bhojani amesema lengo la kutoa nguo hizo ni kusaidia watoto wa mahitaji maalum ili nao waweze kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr kwa furaha kama watoto wengine.

Amesema nguo hizo zimekabidhiwa kwa madiwani wa kata zenye vituo vya watoto wa mahitaji maalum ili wazisambaze kwa wahusika na kuhakikisha zinawafikia walengwa.

Aidha, amewataka madiwani kuendelea kuwa karibu na wananchi kwa kuwasaidia na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amempongeza Diwani Bhojani kwa moyo wake wa kujitolea kusaidia makundi maalum katika jamii.

Sidde amesema vitendo vya kusaidia wenye uhitaji vina mchango mkubwa katika kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuleta faraja kwa makundi yenye changamoto.

Naye Diwani wa Kata ya Msongola, Magdalena Thomas, amemshukuru Bhojani kwa msaada huo na kusema katika kata yake kuna kituo kikubwa cha watoto wa mahitaji maalum, hivyo anaeleza ataenda kugawa nguo hizo ili kuwafikia watoto hao kwa wakati wa sikukuu.