March 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PASS Trust,Stanbic wasaini makubaliano ya yakuunga mkono biashara za kilimo

Na Penina Malundo,Timesmajira

Benki ya Stanbic Bank Tanzania na PASS Trust wamesaini makubaliano ya dhamana ya mikopo ya miaka mitatu yenye lengo la kupanua upatikanaji wa fedha pamoja na kuimarisha ushirikiano katika ufadhili wa miradi ya kijani inayounga mkono biashara za kilimo zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi na mbinu endelevu za kilimo.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini,jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa PASS Trust, Adam Kamanda alisema makubaliano hayo yameundwa kushughulikia changamoto katika sekta ya Kilimo kwa kuanzisha mifumo ambayo itahamasisha taasisi za fedha kuongeza utoaji wa mikopo kwa biashara za kilimo.

Amesema makubaliano hayo yatawezesha mkopaji mmoja ndani ya mnyororo wa thamani wa kilimo kupata mkopo wa hadi shilingi bilioni 10.

“Licha ya umuhimu wa sekta hii ambayo inachangia takribani asilimia 26 ya Pato la Taifa (GDP) na kuajiri asilimia 65 ya nguvu kazi, kilimo bado kinakabiliwa na pengo kubwa la ufadhili, huku wakulima wengi na biashara za kilimo wakishindwa kupata mikopo rasmi kutokana na hatari zinazodhaniwa kuwepo katika utoaji wa mikopo kwa kilimo.

” PASS itatoa mifumo ya kugawana hatari pamoja na utaalamu wa sekta hiyo, wakati Stanbic Bank itachangia uwezo wake wa kifedha na mtandao wake mpana ndani ya sekta ya benki,”amesema

Kamanda amesema kuwa mahitaji ya ufadhili kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) za kilimo yanaendelea kuongezeka kadri sekta hiyo inavyobadilika na kujiunganisha na masoko ya kikanda na kimataifa.

Amesema kuwa kuboresha upatikanaji wa fedha kwa sekta ya kilimo kunatambuliwa sana kama kichocheo muhimu cha kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, na kukuza ukuaji wa uchumi jumuishi.

“Kilimo ni miongoni mwa sekta inayosaidia maisha ya mamilioni ya Watanzania, ushirikiano unaoimarisha mfumo wa ufadhili wa kilimo ni muhimu katika kufungua uwezo kamili wa sekta hii,”amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Suluhisho za Biashara wa Stanbic Bank, Stephen Mpuya amesema kuwa licha ya umuhimu wa kilimo na mnyororo wake wa thamani, upatikanaji wa fedha bado ni mdogo sana.

Ameeleza kuwa kulingana na takwimu za Bank of Tanzania, ni takribani asilimia 12 hadi 13 tu ya mikopo yote inayotolewa na taasisi za fedha inaelekezwa katika sekta ya kilimo.

Ameongeza kuwa mara nyingi biashara ndogo na za kati za kilimo hulazimika kutoa dhamana ya hadi asilimia 125 ya thamani ya mkopo, jambo linalokuwa kikwazo kwa wajasiriamali wengi wenye uwezo.

“Kupitia mpango huu, PASS itatoa dhamana ya kati ya asilimia 50 hadi 60 na inaweza kufikia hadi asilimia 80 ya mkopo,”amesema.