March 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawekeza zaidi ya bil.32 Maabara ya Mkemia Mkuu

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema imewekeza  zaidi ya  bil.32.25 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo mikubwa 32 pamoja na vifaa saidizi 542, ili kuimarisha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara nchini.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 11,2026  na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelis Mafumiko, wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana mwaka 2025/26 ambapo amesema mitambo hiyo imeongeza uwezo wa maabara kufanya uchunguzi wa kisayansi kwa haraka na kwa ubora zaidi, hali inayosaidia kutoa huduma bora kwa wananchi.

Dkt. Mafumiko amesema kuwa katika kipindi cha Januari 2025 hadi Februari 2026, Mamlaka hiyo ilifanikiwa kufanya uchunguzi wa kisayansi wa jumla ya sampuli 247,286.

Ameeleza kuwa ongezeko la sampuli hizo limetokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi na wadau kuhusu huduma zinazotolewa na Mamlaka pamoja na kuboreshwa kwa ubora wa huduma za uchunguzi wa kimaabara.

Pamoja na hayo Dkt.Mafumiko amesema bado Mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto ya kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kufanya matengenezo ya baadhi ya mitambo mikubwa ya maabara, hali inayochangia kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa vifaa hivyo.

“Licha  ya wataalamu wa ndani kuendelea kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo kinga ya baadhi ya mitambo na vifaa vya maabara, bado kuna utegemezi wa wataalamu wa nje katika kushughulikia mitambo mikubwa na ya kisasa.

“Ingawa wataalamu wetu wa ndani wamekuwa wakifanya matengenezo ya kawaida na matengenezo kinga ya baadhi ya mitambo, bado tunalazimika kuwaita wataalamu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matengenezo ya mitambo mikubwa, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji,” amesema Dkt. Mafumiko.

Hata hivyo amesema Mamlaka hiyo inaendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani ili waweze kufanya matengenezo ya mitambo hiyo hapa nchini.

“Tunaendelea kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi wetu ili wawe mahiri na wabobevu katika kufanya matengenezo na matengenezo kinga ya mitambo, hatua itakayopunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi,” amesema.