March 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Absa nchini yalenga kuwezesha wasichana 5,000 kupata ujuzi wa AI kupitia mpango wa ElevateHer

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Benki ya Absa Tanzania, kwa ushirikiano na Microsoft na Women in Tech, imezindua rasmi Mpango wa ElevateHer AI nchini Tanzania, ambao unalenga kuwawezesha wasichana 5,000 wa Kitanzania kupata ujuzi na cheti cha Akili Mnemba (AI).

Mpango huu ni sehemu ya juhudi pana za kiafrika zinazolenga kutoa mafunzo kwa wanawake 50,000 barani Afrika ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi.

Kupitia mpango wa ElevateHer, washiriki watapata fursa ya kujifunza mtandaoni kwa njia ya kujitegemea bila malipo, ambapo watapata maarifa ya msingi ya AI, matumizi ya AI katika biashara, na maendeleo ya taaluma katika mazingira ya kazi yanayoendeshwa na teknolojia ya AI.

Mpango huu utakuwa wazi kwa mwaka mzima.Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya Absa Tanzania,Oscar Mwamfwagasi, amesema mpango huu unaakisi dhamira ya benki kuhakikisha wasichana wanapata ujuzi wa kidijitali unaohitajika kwa siku za usoni.

“Artificial intelligence inabadilisha jinsi uchumi unavyofanya kazi na jinsi watu wanavyofanya kazi.

Kupitia Mpango wa ElevateHer AI, Benki ya Absa Tanzania inalenga kuhakikisha wasichana wa Kitanzania wanapata ujuzi na kujiamini kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali na kuchangia ubunifu na ukuaji.”

Juhudi hii inaendeleza michango ya Absa Tanzania ya kukuza ushiriki wa wanawake katika teknolojia, ikiwa ni pamoja na GirlCode Hackathon ya mwaka jana, ambapo wasichana wabunifu walikusanyika ili kutengeneza suluhisho za kiteknolojia.

Mpango wa ElevateHer unatoa njia tatu za kujifunza: AI kwa Wote, AI kwa Biashara, na AI kwa Ukuaji wa Kitaaluma, na kutoa fursa kwa washiriki kujenga maarifa ya vitendo na kutumia zana za AI katika safari zao za kitaaluma au za ujasiriamali.

Tiara Pathon, Mkurugenzi wa Ujuzi wa AI katika Microsoft Elevate, Microsoft Afrika Kusini, amesema upatikanaji wa ujuzi wa kidijitali kwa kila mmoja ni muhimu kwa ushiriki wa Afrika katika uchumi wa AI duniani.

“Ukuaji wa uchumi jumuishi katika zama za AI unahitaji kujenga ujuzi kwa wingi katika masoko yanayokua. Kwa Afrika, hii inamaanisha kuwekeza kwa makusudi katika ujuzi wa kidijitali na AI kwa wanawake.

Kupitia ushirikiano wetu na Absa na Women in Tech, mpango wa ElevateHer unawawezesha wanawake barani kote kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika kazini na kuimarisha nafasi ya Afrika katika ajira za baadaye.”

Mpango huu pia unasaidiwa na Women in Tech Global, shirika linalojitolea kuwawezesha wanawake na wasichana milioni tano katika Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati (STEM) kufikia mwaka .