


Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Kongwa
WANAWAKE wa Tawi la TUGHE Wizara ya Mifugo na Uvuvi wametumia Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kutoa wito kwa wanawake kujikita katika shughuli za kiuchumi na kuwalea wasichana katika misingi ya kujitegemea ili kuwa mama bora wa baadaye.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika wilayani Kongwa mkoani Dodoma, Katibu wa Tawi la TUGHE Wanawake Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Grace Mwaiselage, alisema wanawake wote waendelee kuwaelimisha wasichana kuhusu umuhimu wa kujishughulisha na shughuli za maendeleo tangu wakiwa na umri mdogo ili waweze kujitegemea na kuchangia ustawi wa familia na jamii kwa ujumla huku akisema hao ndiyo akina mama wajao.
Aliwashukuru wanawake kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki siku hiyo muhimu inayotambua mchango wa wanawake katika jamii.
Mwaiselage pia aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu pamoja na Mradi wa Programu ya Uendelezaji Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji katika Ukanda wa Pwani (TASFAM) kwa kusaidia kufanikisha maadhimisho hayo.
Alisema mradi huo unatoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wanawake ikiwemo miradi ya ufugaji wa samaki ambayo inaweza kuwasaidia wanawake kujipatia kipato na kuboresha maisha ya familia zao.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Tawi hilo, Joyce Mamkwe, alisema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inalenga kujumuisha wanawake katika mnyororo mzima wa thamani ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.
Mamkwe alisema wanawake wanatarajia kunufaika na mradi wa TASFAM ambao una lengo la kuwawezesha kiuchumi na kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Aliongeza kuwa wanawake wa tawi hilo wako tayari kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inaleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Naye Afisa kutoka Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Teddy Salema, aliishukuru wizara kwa kuwapa kibali cha kushiriki katika maadhimisho ya siku hiyo muhimu kwa wanawake.
Salema alizihimiza taasisi nyingine kuiga mfano wa mradi wa TASFAM kwa kuweka kipaumbele katika uwezeshaji wa wanawake kwani wakipewa nafasi wana uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo katika jamii.
Alisema wanawake katika sekta ya mifugo wanafanya vizuri katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufugaji, utoaji wa chanjo pamoja na uzalishaji wa malisho na vyakula vya mifugo.
“Wanawake wengi wanashiriki katika uzalishaji wa malisho na wako mstari wa mbele kuhakikisha mifugo inapata chakula bora, jambo linalosaidia upatikanaji wa nyama na maziwa bora pamoja na kuboresha afya ya mifugo na kuongeza pato la taifa,” alisema.
Alisisitiza kuwa wanawake wakipewa fursa na kuwezeshwa wanaweza kufanya mambo makubwa na kuleta maendeleo makubwa katika taifa.

More Stories
Moto waua watatu wa familia moja Katavi
Wahariri waipongeza REA usambazaji wa Gesi Asilia Lindi,Pwani
Dkt.Kimaro:Hakuna serikali inayoweza kuwaajili wahitimu wote wanaomaliza Shule