September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaelezea Mradi wa Umeme Rusumo

Veronica Simba,TimesMajira Online. Ngara

SERIKALI imeeleza kuwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera, unaotekelezwa Rusumo wilayani Ngara una manufaa mtambuka kwa Watanzania.

Hayo yameelezwa juzi na timu ya Serikali ya Tanzania inayosimamia mradi huo ikihusisha Wakurugenzi wa Bodi na Kamati ya Ufundi, wakiwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya kijamii, inayotekelezwa kupitia mradi husika.

Akizungumza baada ya ziara hiyo kiongozi wa timu hiyo, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Mjumbe wa Bodi wa Kamati husika amesema mbali na umeme, mradi huo utawanufaisha Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya kijamii, ambayo iko katika hatua nzuri za utekelezaji.

Mhandisi Luoga ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, amesema miradi ya kijamii inayotekelezwa ni pamoja na inayohusu sekta za afya, elimu, maji, mifugo na kilimo.

Akizungumzia lengo la timu hiyo kutembelea miradi ya kijamii inayoendelea kutekelezwa, Mhandisi Luoga amesema ni kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wake, kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati.

“Tumetembelea shule za msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya na miradi ya maji ambayo yote inayotekelezwa hapa Ngara na tumejiridhisha kuwa kwa sehemu kubwa, imefkia hatua nzuri na baadhi yake imekamilika,” amesema.