Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online-Shinyanga
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewataka wananchi kutogombana kwa sababu ya itikadi za vyama vyao vya siasa na badala yake wadumishe upendo.
Kihongosi amesema hayo, Machi 6, 2026 mkoani Shinyanga, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Town, uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, akihutubia na kutatua kero za wananchi wa eneo hilo.
“Itikadi za vyama vya siasa isitupelekee katika machafuko yatakayoharibu amani ya nchi yetu, vyama vipo, vitapita lakini Tanzania itabaki,”amesema Kihongosi na kuongeza:
“Msigombane kwa itikadi za vyama vyetu, tupendane kwa utanzania wetu, hata mtu akifa yupo anayezikwa na chama cha siasa?, au unazikwa na watu, watu ndio wanakwenda kukuzika na hata ukienda mbinguni hautaulizwa wewe ni chama gani, bali yataangaliwa matendo yako,”.
“Sasa pendaneni msingombane, msichukiane kwa sababu yule ni CUF, ACT/Wazalendo, CCM, NLD, DP au CHAUMA wote tupo ndani ya taifa moja hivyo tuwe kitu kimoja,”.
Pia amesema kuwa, vipo baadhi ya vyama vya siasa vimeonekana kuhamasisha uvunjifu wa amani, hivyo amewataka wananchi kuwapuuza badala yake waendelee kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano.
“Kuna watu wapo radhi nchi iangamie ili wao wafanye mambo ya hovyo jambo ambalo CCM hatutalikubali hata dakika moja, tutailinda nchi yetu, tutawahamasisha wananchi kuimarisha umoja wa kitaifa, upendo, mshikamano ili vizazi vijavyo vikute Tanzania iliyo bora kama sisi tulivyorithi kwa wazee,”amesema Kihongosi.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi