March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake wahimizwa kuchangamkia fursa za kiuchumi

Fresha Kinasa, TimesMajiraonline, Mara.

WANAWAKE wametakiwa kuzitumia vyema fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya ujasiriamali na mikopo nafuu inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri, kusudi waweze kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na kupambana na ukatili wa kijinsia mkoani Mara, Rhobi Samwelly, ameyasema hayo Machi 6, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake wilayani Rorya mkoani Mara.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Kata ya Koryo, kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Utegi, na kuhudhuriwa na makundi mbalimbali ya wanawake kutoka sekta binafsi, taasisi za umma, serikalini pamoja na wananchi wa wilaya hiyo.

Ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Haki kwa Wanawake na Wasichana, Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira 2050.”

Rhobi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Hassan imeendelea kutoa fursa ya mikopo nafuu kwa wanawake. Hivyo, ni muhimu wakachangamkia fursa hiyo ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kufanya shughuli mbalimbali za biashara na ujasiriamali zenye tija.

Pia amewataka wanawake wilayani humo kutumia siku hiyo muhimu kujitathmini na kuimarisha malezi bora kwa watoto wao, kwani wana nafasi nzuri ya kuimarisha malezi, makuzi sambamba na kusimamia maadili mema yatakayowasaidia watoto kukua katika mazingira salama na yenye heshima.

Aidha, amesisitiza wanawake kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, akieleza kuwa ukatili unaathiri maendeleo ya watoto kimwili, kiakili na kisaikolojia. Huku akihimiza wazazi na walezi kuwalinda watoto na kuwapa malezi yenye upendo wakizingatia haki za watoto ili kuwasaidia kufikia ndoto zao za baadaye

“Wanawake tukijiimarisha kiuchumi tutaweza kusaidia familia zetu, kuwapatia watoto mahitaji muhimu na kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa letu kwa ujumla,” amesema Rhobi.

Akisoma risala ya wanawake wa Wilaya ya Rorya, Lilian Fransisco ambaye ni Mratibu wa Dawati la Wanawake Wilaya ya Rorya, amesema anaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwathamini wanawake na kutatua changamoto zao mbalimbali kwa juhudi na mikakati endelevu.

“Tunaishukuru serikali yetu, kwa Sasa wanawake tunayo nafasi ya kupiga hatua kimaendeleo kwani changamoto nyingi serikali imeendelea kuzitatua kusudi tuendelee kuwa mstari wa mbele katika a ya uongozi, uzalishaji mali na kufikia usawa katika nyanja mbalimbali.”amesema Lilian