March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CAMFED kuendelea kutimiza ndoto za watoto wa kike

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Mbeya

SHIRIKA lisilo la kiserikali linalojikita katika kusaidia elimu ya mtoto wa kike kutoka katika mazingira magumu, CAMFED – Campaign for Female Education Development, limesema linaendelea kuwekeza katika kuwafadhili wanafunzi wa kike ili kuwawezesha kupata elimu bora na kujikwamua katika changamoto za kimaisha zinazopelekea wengi wao kukatisha masomo.

Kauli hiyo imetolewa Machi 2, 2026 na Neema Msemwa, Ofisa wa CAMFED mkoa wa Iringa, wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa wanafunzi 73 wa vyuo vikuu kutoka wilaya mbalimbali nchini, ambao wanasomeshwa na shirika hilo katika vyuo vinavyopatikana mkoani Mbeya.

Msemwa amesema kuwa lengo kuu la CAMFED ni kuhakikisha kila mtoto wa kike anapata fursa sawa ya elimu bila vikwazo, akibainisha kuwa wengi wanaotoka kwenye mazingira hatarishi hukabiliwa na unyanyasaji wa nyumbani, utoro, na kulazimika kufanya kazi za ndani kutokana na kukosa msaada wa mahitaji ya msingi ya shule.

“Katika kutekeleza dira yetu, tunaanza kwa kumpeleka shule yule mwenye changamoto kubwa zaidi. Tunampa mahitaji yote muhimu kama sare, madaftari, ada, na kwa wanaotoka mbali, tunanunua baiskeli ili waweze kufika shuleni bila usumbufu,” amesema.

Msemwa: Mimi ni zao la CAMFED

Msemwa amesema kuwa CAMFED imekuwa msaada mkubwa kwa watoto wa kike tangu ianze kutoa ufadhili nchini mwaka 2006, akibainisha kuwa yeye ni mmoja wa wanufaika wa mpango huo.

“Nimetoka kwenye mazingira magumu, baba yangu hakuwepo, lakini CAMFED ilinifadhili hadi kumaliza chuo kikuu. Huu ni ushahidi kwamba tunamtoa mtoto kutoka kukosa hata daftari hadi kuwa kiongozi wa mabadiliko,” amesema.

Amesema, hadi sasa CAMFED imeshasomesha zaidi ya wanafunzi wa kike 60,000, ambapo baadhi wameajiriwa, wengine wamejiajiri, na wengine wanafanya shughuli mbalimbali za kujikimu na kusema kwa ngazi ya vyuo vikuu, shirika linawafadhili zaidi ya wanafunzi 1,104 nchi nzima.

Elimu ya Fedha na Kujitambua

Msemwa amesema kuwa ziara ya CAMFED mkoani Mbeya imejikita kutoa mafunzo ya kujitambua, elimu ya fedha, namna ya kuweka akiba na ujasiriamali, ili kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na changamoto za ajira na kuwapa uwezo wa kujitegemea.

“Tumeweka mkazo kwao kubaki vyuoni, kuepuka vishawishi, na kujitoa kwenye safari ya kuwa viongozi wa kesho,” amesema.

Ameongeza kuwa CAMFED inafanya kazi katika mikoa 10 nchini, na mafunzo hayo yamekusanya wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali ili kuwajengea mtandao wa marafiki na fursa.

Shirika lapanua ufadhili wake Vyuo Vikuu 66

Kwa upande wake, Stephano Lunyungu, Ofisa Fedha wa CAMFED, amesema shirika linalenga kusaidia watoto wa kike kuanzia elimu ya sekondari hadi vyuo vikuu. Hadi sasa lipo katika vyuo 66 nchini, na mkoani Mbeya pekee linawaunga mkono wanafunzi 76 katika vyuo vinne: TEKU, Mzumbe, Catholic University na Chuo cha Uhasibu Mbeya (MUST).

Amesema kwa wale waliomaliza masomo, shirika lina programu za ujasiriamali zinazowawezesha kuanzisha shughuli zao kama biashara na kilimo ili kujitegemea.

Wanufaika waeleza furaha yao

Antonia Emmanuel, mwanafunzi wa Catholic University kutoka Singida, amesema CAMFED imemtoa mbali kwa kumpatia elimu kuanzia kidato cha kwanza hadi chuo kikuu.

“Sikuwa na ndoto ya kusoma sekondari kutokana na ugumu wa maisha, lakini CAMFED wamekuwa wakinilipia kila kitu hadi leo nipo mwaka wa pili chuoni. Wamenipa maisha mapya,” amesema.

Naye Diana Eliazari, mwanafunzi wa MUST kutoka Nyamagana mkoani Mwanza, amesema alisaidiwa na shirika hilo tangu mwaka 2008 na sasa anaendelea na masomo ya chuo kikuu.

“Tunaliomba shirika liendelee kutuunga mkono. Limetutoa mbali na limetupa matumaini mapya ya kuendelea na masomo na kuwa wanawake wenye mchango kwenye jamii,” amesema.