Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) imesema katika kipindi cha mwaka mmoja imefanikiwa kuanzisha huduma mpya tisa za kibobezi ambazo hapo awali ziliwalazimu wagonjwa kuzifuata nje ya Tanzania.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 2,2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Balozi Dkt.Mpoki Ulisubisya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya MOI katika kipindi cha mwaka mmoja.
Dkt.Ulisubisya ametaja huduma hizo kuwa ni pamoja na upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili unde, upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu, huduma ya kuchukua sampuli za vipimo kwa njia ya matundu pamoja na huduma ya kuweka tiba simenti kwenye pingili za mgongo zilizovunjika.

“Huduma zingine ni za tiba ya maumivu, huduma ya upasuaji rekebishi wa viungo vilivyopooza, huduma ya upasuaji wa uvimbe na ubongo kwa kutumia teknolojia ya fluorescein na kuanza kwa wodi mpya za kisasa za ‘premier’ kwa ajili ya wagonjwa maalum na wakimataifa ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa maalum na wakimataifa,”amesema.
Aidha Dkt.Ulisubisya ameeleza kuwa Taasisi ya MOI imeendelea kutoa huduma nyingine za kibingwa Bobezi na kupunguza rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi ikiwemo upasuaji na uchunguzi wa mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu pamoja na upasuaji wa nyonga na magoti wa marudio ambapo wagonjwa 31 wamepatiwa matibabu hayo.
“Huduma nyingine za kibingwa ni matibabu ya kiharusi kwa kupitia mishipa mikubwa ya damu, upasuaji wa kunyoosha mgongo uliopinda, kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia tundu la pua, huduma ya maumivu sugu ya mgongo, huduma ya wagonjwa maalum na wagonjwa wa kimataifa,”amesema.
Pia ametaja wagonjwa wa kimataifa waliohudumiwa ni kutoka mataifa ya Congo, Comoro, Uganda, South Sudan, Burundi na mataifa mengine nje ya bara la afrika.
Vilevile amesema MOI inatoa huduma ya mkono wa umeme na kutengeneza viungo bandia kwa kutumia teknolojia ya 3D, upandikizaji wa nyonga bandia, upandikizaji wa goti bandia, upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo pamoja na upasuaji wa mfupa wa kiuno.
“Katika kipindi cha mwaka mmoja, Taasisi ya MOI imefanikiwa kutoa huduma za kibobezi wa wagonjwa 2,228 ambapo huduma hizo zimeiwezesha MOI kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi,”amesema.

Pamoja na hayo Dkt.Ulisubisya amesema MOI imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la kuonea wagonjwa wa nje (OPD) unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 13.8 ambapo ukikamilika utapunguza msongamano wa wagonjwa katika OPD ya sasa kwani zaidi ya wagonjwa 1500 wataweza kuhudumiwa kwa siku.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama