Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
MKUU wa Wilaya ya Mbeya,Solomon Itunda, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuthamini na kushirikiana na taasisi za kidini katika kukuza maadili, kuimarisha amani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza Februari 28, 2026 katika kongamano la wanawake wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Itunda amewapongeza wanawake wa CCT kwa kuandaa kongamano muhimu lililowakutanisha washiriki kutoka mikoa zaidi ya 13 nchini. Alisisitiza kuwa mchango wa wanawake katika maombi, maadili na malezi ya vizazi ni nguzo kubwa katika kuijenga Tanzania yenye amani, mshikamano na hofu ya Mungu.
Itunda amesema lengo la kongamano hilo ni kuliombea Taifa na Kanisa kwa ujumla, akibainisha kuwa maombi ya kitaifa ni msingi muhimu wa kuimarisha umoja wa kitaifa na ustawi wa wananchi.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesisisitiza kuwa wanawake ni nguzo ya Taifa na wana nafasi ya kipekee katika kulea kizazi chenye uzalendo, maadili na nidhamu.
Katika hotuba yake, Itunda amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza ushirikiano na viongozi wa dini nchini kupitia falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Mpya).
Amesema falsafa hiyo imeendelea kuimarisha mshikamano wa kitaifa, uvumilivu na mazingira ya amani yanayowezesha maendeleo.
Vilevile, ameshukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuhubiri amani na utulivu, akibainisha kuwa Mkoa wa Mbeya utaendelea kuwa kitovu cha mikutano na makongamano ya kitaifa kutokana na mazingira yake tulivu na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na taasisi za kidini.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini akiwemo Askofu wa Dayosisi ya Konde wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Baba Askofu Gefrey Mwakihaba,Askofu wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mbeya; Askofu wa Kanisa la Anglikana,pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Canon Dkt. Moses Matonya.
Kongamano hilo la kitaifa limehitimishwa kwa maombi maalum ya kuliombea Taifa, viongozi wa Serikali na Kanisa, pamoja na kuhimiza umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania huku Serikali ikiendelea kutambua na kuthamini mchango wa wanawake wa CCT katika kujenga Taifa lenye maadili na hofu ya Mungu.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina