Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Wizara yake haitavumilia watumishi wazembe wasio na nia ya kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo, akisisitiza kuwa uwajibikaji ni msingi wa kuboresha huduma za maji kwa wananchi.
Aweso ametoa kauli hiyo leo, Februari 27, 2025, wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Vyombo vya Watoa Huduma za Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs), uliofanyika katika Ukumbi wa Jiji Mtumba, jijini Dodoma.
Amesema Wizara inahitaji watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi na bidii ili kuleta matokeo chanya, ikiwemo kuboresha huduma za maji na kuondoa changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Wizara inahitaji watumishi wanaofanya kazi kwa kuleta matokeo, ambayo ni kuboreka kwa huduma za maji kwa wananchi na kuondoa changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo,” amesema Aweso.
Aidha, amepongeza vyombo hivyo kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha jamii zinapata huduma ya maji safi na salama, akibainisha kuwa vinafanya kazi muhimu katika kusimamia miradi ya maji vijijini.
Aweso amesema jumuiya hizo zinatambulika kisheria nchini, hivyo zina wajibu wa kuhakikisha maeneo yenye changamoto katika utoaji wa huduma za maji yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Kutokana na hali hiyo, amezitaka CBWSOs kuongeza juhudi katika utunzaji wa mazingira na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa huduma za maji katika maeneo wanayoyahudumia, ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unaendelea kuwa wa uhakika na endelevu.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama