April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATCL kununua Ndege nane zaidi, mapato yafikia Dola Milioni 157

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

SERIKALI imesema ina mpango wa kununua ndege nane zaidi, huku ndege nne aina ya Dash 8 Q400 zikiwa katika hatua mbalimbali za manunuzi ambapo mbili zipo katika hatua ya zabuni na mbili katika hatua ya kibali.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam mapema leo Februari 26,206 na Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa wakati akizugumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhusiana na mafanikio sekta ya usafiri na usafirishaji.

Amesema kukamilika kwa mchakato huo kutafanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 28 ambapo katika mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilikamilisha ununuzi wa ndege aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyowasili Agosti 20, 2024, hatua iliyofanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 16.

“Serikali imeendelea kuwekeza katika ununuzi wa ndege mpya, kuboresha karakana za matengenezo, kuimarisha mazingira ya kazi pamoja na kutekeleza mikakati ya kuongeza ubora, usalama na ufanisi katika utoaji wa huduma za usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya anga”amesema

Kwa upande wa mafanikio Msigwa amesema uwekezaji huo umeiwezesha ATCL kuongeza idadi ya abiria kutoka 822,232 mwaka 2021/22 hadi kufikia abiria 1,178,025 mwaka 2024/25.

Amesema Katika kipindi cha nusu mwaka pekee kuanzia Julai hadi Desemba 2025, ATCL ilisafirisha abiria 709,432.

Kwa upande wa mizigo, usafirishaji umeongezeka kutoka tani 2,567 mwaka 2021/22 hadi tani 6,919 mwaka 2024/25, ongezeko lililochangiwa na ununuzi wa ndege ya mizigo na upanuzi wa safari za kimataifa na kikanda, hatua iliyorahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, mbogamboga na matunda kwenda masoko ya nje.

Ameongeza kuwa , mchango wa ATCL katika uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika ambapo katika mwaka 2024/25 shirika hilo lilikusanya dola za Marekani milioni 157.69, sawa na ongezeko la asilimia 87.88 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Amesema katika kipindi hicho, ATCL ilichangia Shilingi bilioni 52.35 kama kodi, ada na tozo mbalimbali za kisheria.

Msigwa aliongeza kuwa kampuni hiyo imepanga kuanzisha safari mpya kuelekea Seychelles, Muscat na Jeddah kabla ya Juni 2026, hatua itakayofungua fursa zaidi za biashara kimataifa.

Kwa upande wa ajira,amesema ATCL imeongeza watumishi kutoka 826 mwezi Juni 2024 hadi kufikia 1,031 mwezi Desemba 2025.

Aidha, watumishi 356 wamepatiwa mafunzo maalum ili kuongeza ujuzi na tija katika kada za urubani, uhandisi wa ndege na masuala muhimu ya usafiri wa anga.