March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NBI na Rusumo Power Company wasaini MoU kuimarisha uendelevu kupitia Ufuatiliaji na Utabiri Bora wa Maji ya Mito

Na Penina Malundo,Timesmajira

USHIRIKIANO wa kikanda wa Nchi Wanachama 10 ujulikanao kwa jina la Nile Basin Initiative (NBI), kwa niaba ya taasisi za maji za kitaifa za Burundi, Rwanda na Tanzania, imesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Kampuni ya Rusumo Power Company kwa lengo la kuimarisha uendelevu na ufanisi wa Mradi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Maji cha Maporomoko ya Rusumo (Regional Rusumo Falls Hydroelectric Project).

Mradi huo wa kimkakati wa kuvuka mipaka unatoa nishati safi kwa takribani watu milioni moja katika nchi hizo tatu.

NBI imesaini MoU hiyo kwa niaba ya Taasisi ya Jiografia ya Burundi (IGEBU), Bodi ya Rasilimali za Maji ya Rwanda (Rwanda Water Resources Board) na Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria Tanzania (Lake Victoria Basin Water Board), kwa lengo la kuhakikisha uendelevu na uboreshaji wa mradi kupitia ufuatiliaji wa kisasa wa takwimu za maji (hydrological monitoring).

Mfumo huo utahusisha uzalishaji wa taarifa za papo kwa papo (real-time) na za utabiri kuhusu viwango vya maji ya mito, maziwa pamoja na ubora wa maji.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa NBI, Dkt. Mhandisi Nestor Niyonzima, amesema wamepiga hatua muhimu kwa niaba ya Burundi, Rwanda na Tanzania — nchi ambazo zinazomiliki na kuendesha kwa pamoja Rusumo Power Company Ltd — katika kuhuisha mradi ulioanzishwa kupitia juhudi za pamoja za Nchi Wanachama kwa lengo la kuendeleza uwekezaji wa kijamii na kiuchumi katika Mto Nile kwa ustawi wa pamoja.

“MoU hii itasaidia kukabiliana na changamoto tatu kuu zinazoikabili mitambo ya kuzalisha umeme: upungufu wa takwimu sahihi za maji kwa ajili ya upangaji na usimamizi bora wa uzalishaji wa umeme; mzigo mkubwa wa mashapo unaosababishwa na mmomonyoko wa udongo; na magugu vamizi ya maji aina ya gugu maji (water hyacinth), ambapo takribani tani 15 hufika kwenye kituo cha umeme kila siku,”amesema

Makubaliano hayo pia yanahusisha uendeshaji na matengenezo ya vituo sita vya kikanda vya ufuatiliaji wa maji vilivyoanzishwa na NBI kwa kushirikiana na nchi hizo tatu na kampuni ya umeme katika eneo la Rusumo. Vituo hivyo vipo katika mito ya Ruvubu (Burundi), Ruvuvu (Tanzania), Akagera (Rwanda) na Kagera (Tanzania).

Aidha, MoU inajumuisha mfumo wa kubadilishana takwimu na taarifa kati ya nchi hizo tatu kupitia mfumo maalum wa kidijitali (web-based application) uliotengenezwa na NBI kwa ushirikiano na Nchi Wanachama pamoja na Rusumo Power Company Ltd.

Kupitia makubaliano hayo, Burundi, Rwanda na Tanzania zitakuwa zinazalisha na kushirikiana takwimu za maji kwa wakati, zenye ubora na uhakika, zitakazosaidia moja kwa moja katika upangaji na maamuzi ya uendeshaji wa kituo cha umeme.

Ufuatiliaji ulioboreshwa pia utachangia suluhisho la muda mrefu dhidi ya mashapo na gugu maji, sambamba na matumizi ya mbinu rafiki kwa mazingira katika maeneo ya vyanzo vya maji.Mkurugenzi Mkuu wa IGEBU na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kiufundi ya Nile (Nile Technical Advisory Committee),Augustin Ngenzirabona, amesema Rusumo ni alama ya ushirikiano unaotekelezwa kwa vitendo — ni mfano wa manufaa ya pamoja, ustawi wa pamoja na ujumuishaji wa kikanda.Alisema ni muhimu kuhakikisha mitambo inaendelea kufanya kazi na kulinda uwekezaji huo wa pamoja kupitia usimamizi bora wa bonde la maji.

”Chini ya MoU hiyo, Rusumo Power Company Ltd pamoja na nchi tatu zitachangia kwa pamoja gharama za uendeshaji, matengenezo na majukumu mengine yanayohusiana na utekelezaji wa makubaliano,”amesema.

NBI ina matumaini kuwa mpango huu utakuwa mfano kwa mabonde mengine ya mito barani Afrika na duniani, kwa kuonesha umuhimu wa uendeshaji wa pamoja, mifumo shirikishi ya taarifa na ufadhili endelevu wa miundombinu ya kuvuka mipaka.

Vituo sita vya ufuatiliaji vilivyotajwa katika MoU ni sehemu ya Mfumo wa Kikanda wa Ufuatiliaji wa Maji wa Bonde la Nile (Nile Basin Regional Hydrological Monitoring System) ulioanzishwa na NBI kwa kushirikiana na Nchi Wanachama wake, kwa msaada wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani (BMZ) na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Shirika la GIZ.

GIZ inaendelea kuunga mkono mfumo huo wa kikanda pamoja na kazi za NBI za kuratibu mabwawa mfululizo katika Bonde la Nile na Programu ya Uwekezaji ya Bonde la Mto Nile.–