



Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MKURUGENZI wa Children in Crossfire (CiC), Craig Ferla, amesema mustakabali wa Tanzania uko mikononi mwa watoto wa sasa na vizazi vinavyokuja, akisisitiza umuhimu wa kuelekeza nguvu zote katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Akitoa wasilisho wakati wa ufunguzi wa mkutano wa programu ya elimu ya awali uliofanyika jijini Dodoma, Ferla amesema pamoja na kizazi cha Gen Z kinachoonekana kwa sasa, kuna vizazi vingine kama kizazi Alpha, Beta na Gamma vinavyokuja ambavyo ni hazina muhimu ya Taifa siku za usoni.
Alisema Tanzania imejizatiti katika kuimarisha maendeleo ya watoto kupitia mikakati ya kisayansi ikiwemo mpango wa kujenga umahiri wa K tatu na Dira ya Taifa ya 2050 inayolenga ukuaji wa ubongo wa mtoto na kufikia utimilifu wao, huku akibainisha kuwa watoto wa awali ni msingi wa kujenga rasilimali watu wenye tija hapo baadaye.
Ferla pia alieleza kuwa ajenda ya watoto imepewa kipaumbele cha juu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza katika kaulimbiu isemayo “Watoto wetu ni tunu yetu” na kwamba hakuna rasilimali yenye thamani kuliko mtoto.
Akifungua mkutano huo ,Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ,Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) aliyewakilishwa na Abdul Maulidi, alilipongeza shirika hilo kwa kushirikiana na serikali kutekeleza mradi huo mkoani Dodoma na kubainisha kuwa sera ya elimu bila ada imeongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa shule za awali kutoka wanafunzi 1,543,843 mwaka 2022 hadi kufikia 1,656,726 mwaka 2025.
Aliongeza kuwa serikali imeboresha mitaala katika ngazi mbalimbali za elimu na inaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia ubora wa ujifunzaji, huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wa elimu na kuimarisha jumuiya za ujifunzaji kwa walimu pamoja na kuhakikisha huduma ya chakula shuleni inakuwa ajenda ya kudumu.
Naye Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Kiduma Mageni, alisema kupitia ushirikiano na Children in Crossfire, mkoa umefanikiwa kujengewa madarasa mapya 33 na kukarabati madarasa ya awali 473, hatua iliyobooresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji hususan katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Aidha, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Shule za Msingi, Ephram Simbeye, alipongeza jitihada za shirika hilo katika kuunga mkono juhudi za serikali kuimarisha sekta ya elimu na kuendeleza agenda ya maendeleo ya mtoto nchini.
Mkutano huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za pamoja za serikali na wadau kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya elimu bora ya awali na kuandaliwa kuwa wananchi wenye tija kwa maendeleo ya Taifa.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina