March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baraza la Madiwani laridhia kuwafukuza kazi watumishi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Rungwe

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya limeazimia kuwafukuza kazi watumishi watatu wa Halmashauri hiyo kutokana na utoro wa muda mrefu kazini.

Uamuzi huo ulitolewa Februari 18, 2026 mbele ya Baraza hilo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Gabriel Mwakagenda, wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mashauri ya kinidhamu yaliyowasilishwa dhidi ya watumishi hao.

Mwakagenda amesema jumla ya mashauri manne yaliwasilishwa katika kikao hicho, ambapo matatu yalithibitika na kusababisha watumishi watatu kufukuzwa kazi, huku shauri moja likirudishwa kwa ajili ya kuanza upya taratibu za kiutumishi kwa mujibu wa sheria.

“Shauri hili moja limerudishwa ili kuanza upya utaratibu wa kupitia mambo muhimu katika utumishi, ili hatua zinazofuata ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Mwakagenda.

Amefafanua kuwa baada ya Baraza kupitia kwa kina mashauri hayo na kujiridhisha, lilifikia uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi watatu kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo utoro wa muda mrefu kazini, huku shauri lililosalia likirejeshwa katika ngazi husika kwa ajili ya kufuata taratibu za utumishi wa umma.

Aidha, Mwenyekiti huyo amewasihi watumishi wa halmashauri hiyo kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesisitiza umuhimu wa nidhamu ya kazi kwa watumishi wote waliokabidhiwa dhamana ya kuwahudumia wananchi.