Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
TAASISI ya Kiislam ya Al-Mallid Dodoma imelalamikia watumishi wa Wizara ya Ardhi, akiwemo Kamishna na Naibu Kamishna wa Ardhi Tanzania waliomtaja kwa jina la Hussein Iddi kwa madai ya kutaka kuwagombanisha na Serikali kufuatia mgogoro wa kiwanja namba 8AY kilichopo Nzuguni C jijini Dodoma.
Malalamiko hayo yalitolewa jijini hapa hivi karibuni na Ustadhi Bakari Mgaza, mjumbe wa Al-Mallid Dodoma, wakati akisoma risala kwa Mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Al-Mallid Taifa, Sheikh Yusuph Kassim Mikidadi, katika hafla ya dua ya kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani sambamba na kuliombea Taifa amani pamoja na viongozi wake.

Hafla hiyo ilifanyika katika eneo la kiwanja hicho ambapo Ustadhi Bakari alidai kuwa Serikali imechukua zaidi ya Sh milioni 140 kutoka kwa waislam hao baada ya kuomba eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, chuo cha uuguzi na nyumba za makazi.
Alidai kuwa kwa sasa kuna mgogoro unaosababishwa na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Ardhi wanaotaka kuwagombanisha na Serikali.
“Mwenyekiti wa Al-Mallid, kiwanja hiki cha waislam waliokitoa kwetu, mamlaka zote kuanzia Wizara ya Ardhi mpaka Jiji la Dodoma kwa kuwadharau waislam na kuwaona wanyonge na kwa makusudi mazima wakijigamba wao ndiyo Serikali wameamua kukigawana kiwanja hiki watumishi wa Ardhi huku wakijua ni matumizi mabaya ya madaraka,” alisema.
Alifafanua kuwa tayari wana kibali cha kumiliki eneo hilo kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) (Kabidhi Wasii Mkuu) na kwamba Halmashauri ya Jiji la Dodoma imemthibitishia Kabidhi Wasii Mkuu kuwa eneo hilo ni mali yao.

Vilevile alisema wana eneo lingine Ihumwa pembezoni mwa reli ya SGR ambalo nalo RITA imewapatia kibali cha kumiliki baada ya Jiji la Dodoma kumwandikia barua Kabidhi Wasii Mkuu kuthibitisha uhalali wao.
Kwa upande wake, Ustadhi Said Maganga, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini Al-Mallid, alisema mgogoro huo umetengenezwa na Mathew, Kamishna wa Ardhi Tanzania, akidai aliagizwa na Waziri Ndejembi alipokuwa kwenye wizara hiyo kuzungumza na Al-Mallid kumaliza mgogoro huo lakini haikuwezekana.
Alisema waliposhindwana naye walimfuata Mwigulu Nchemba ambapo walipewa Naibu Kamishna wa Ardhi aitwaye Hussein, lakini nao hawakufikia muafaka.
Alidai kuwa wamelipa Sh milioni 100, kisha milioni 50, milioni 30, milioni 36 na milioni tisa kupitia control namba mbalimbali na hawadaiwi chochote na Serikali, jumla ikiwa Sh milioni 138.
“Mwisho wa siku Hussein Naibu Kamishna wa Ardhi akatuambia, ‘Nyie si mmeenda kwa Mwigulu, mwambieni awape kiwanja sasa kama anacho,’” alisema.

Aliongeza kuwa baadhi ya watumishi akiwemo Fadhili Mkuu wa Ardhi wanadai maeneo hayo ni ya matumizi ya Serikali wakati wao wameshalipa fedha zote zinazotakiwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Al-Mallid Mkoa wa Dodoma, Sheikh Kayumbo Kabutali, aliwaambia waumini kuwa eneo hilo ni mali yao na hawatakubali kuburuzwa.
Naye Mwenyekiti wa Taifa, Sheikh Mikidadi, alisema amesikia kilio chao na kwamba siyo nia ya Serikali kuwa na migogoro na wananchi bali changamoto ipo kwa baadhi ya watumishi.
“Kwa taarifa na nyaraka nilizozipata naamini kiwanja hiki ni cha waislam. Tutazungumza na wizara husika kuangalia namna ya kumaliza suala hili,” alisema.

Katibu Mkuu wa Taasisi Taifa, Sheikh Rajabu Katimba, alisema walikuwa katika kiwanja hicho kuukaribisha Mwezi wa Ramadhani na kuliombea Taifa, Rais na watumishi wake, huku akisisitiza kuwa kufunga Ramadhani ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu.
Dua ya kuukaribisha Mwezi wa Ramadhani na kuliombea Taifa ilisomwa na Sheikh Hussein Yakubu.
Hata hivyo jitihada za kumpata Naibu Kamishna Hussein Iddi aliyelalamikiwa kusababisha mgogoro huo ili kupata ufafanuzi zilishindakana kutokana na kutopokea simu aliyopigiwa siku mbili mfululizo na kutokujibu ujumbe wa simu uliomtaka atoe ufafanuzi kuhusu mgogoro huo.
Jitihada za kumtafuta bado zinaendelea.






More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina