March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo mpya wa uwajibikaji ahadi za COP unaoweza kutekelezwa Tanzania

Na Martha Fatael, TimesMajira Online

Utangulizi

WATAALAM wa tabianchi na uwajibikaji wanasema Tanzania inahitaji mfumo madhubuti wa kitaifa ili kutimiza kwa ufanisi ahadi zake zinazotolewa katika mikutano ya COP (Mkutano wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi). Mfumo huu unapaswa kuunganisha miradi yote ya tabianchi, ufuatiliaji wa fedha, tathmini ya athari kwa wananchi na ushiriki wa wadau wote.

Kiasi cha fedha Tanzania imepatikana na changamoto za ufuatiliaji

Takwimu za Wizara ya Mazingira na Ofisi ya Makamu wa Rais zinaonyesha kuwa Tanzania ilipata takriban dola za Marekani Milioni 463.31 (sawa na Sh Trilion 1.1) kati ya ahadi yenye thamani ya dola Milioni 782.2 (karibu Sh1.94) zilizotolewa kupitia COP29 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Fedha hizi zinatumika kuanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya kukabiliana na athari za hali ya hewa.

Serikali pia iko katika hatua za kuanzisha idara maalum ya kusimamia ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi, ili kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa fedha hizo.

Kufuatilia fedha za tabianchi kwa ufanisi

Mchambuzi wa Sera za Tabianchi kutoka Climate Action Network Tanzania (CAN Tanzania) Boniventure Mchomvu, anasema changamoto kubwa ni kukosa mifumo madhubuti ya kufuatilia fedha zote zile za serikali na zile za washirika wa maendeleo kutokana na ukosefu wa data zinazoonekana kwa umma.

Takwimu za nyaraka za kitaifa zinaonyesha kuwa licha ya fedha kubwa kuingia kwa ajili ya miradi ya tabianchi, taarifa kuhusu matumizi ya fedha hizo mara nyingi zinabaki kwenye ofisi za wizara na hazionekani wazi kwa wananchi. Hii inathibitisha hitaji la kuweka mfumo wa ufuatiliaji wa fedha (climate finance tracking mechanisms).

Tathmini ya athari za miradi kwa wananchi

Mhadhiri wa Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Patrick Luganda, anasisitiza kuwa Tanzania inahitaji kutumia mfumo wa tathmini ya athari (impact evaluation framework) ili kuhakikisha miradi ya tabianchi inaleta matokeo halisi kwa wananchi, sio tu kuonekana kwenye ripoti za kimataifa.

Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa miradi ya hali ya hewa inayolenga kuongeza uwezo wa kustahimili mafuriko na majanga imesababisha uwekezaji wa karibu dola milioni 300 ambao utafaidisha takriban wananchi milioni 1.9 kwa kuboresha uwezo wa kukabiliana na majanga nchini Tanzania.

Ushirikishwaji wa jamii na wadau wa kiraia

Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais na Mjumbe wa Kikosi cha Majadiliano cha Afrika (AGN)Dkt. Richard Muyungi, alisema bila ushiriki wa wananchi, miradi inaweza kufanyika kisheria lakini isilete manufaa halisi kwa jamii. Ushiriki wa wananchi unaonekana muhimu ili kuhakikisha fedha za tabianchi zinatumika kwa maslahi ya wenyeji.

Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa miradi yenye ushiriki wa jamii mara nyingi inaleta matokeo bora ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kama ulaji bora wa maji, uhifadhi wa ardhi na kilimo endelevu hasa maeneo yenye hatari kubwa kama ukame au mafuriko.

Maoni ya Wananchi wa Moshi

Wakazi wa Manispaa ya Moshi wamesema licha ya kusikia Tanzania imepokea mabilioni ya fedha za tabianchi kupitia mikutano ya COP, bado hawaelewi fedha hizo zinafanya kazi gani kwao moja kwa moja. Mkazi wa Majengo, Neema Shirima, alisema wananchi wengi wanabaki kusikia takwimu kubwa za dola na trilioni lakini hawapewi taarifa rahisi zinazoeleza miradi ipi inatekelezwa katika maeneo yao na ni lini wataona matokeo yake.

Kwa upande wake, mkulima kutoka Kata ya Mabogini, Joseph Mrema, alisema mabadiliko ya tabianchi yameathiri sana kilimo cha migomba na mbogamboga, lakini hajawahi kushirikishwa kwenye mikutano yoyote inayohusu miradi ya tabianchi. Alisema kama fedha hizo zinalenga kuongeza ustahimilivu, basi wakulima wadogo wanapaswa kuwa wa kwanza kupewa taarifa na kushirikishwa katika kupanga vipaumbele vya miradi.

Naye mfanyabiashara wa soko la Memorial,Asha Kimaro, alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa uwazi kuhusu matumizi ya fedha hizo. Alisema wananchi wengi Moshi wanasikia kuhusu COP kupitia vyombo vya habari lakini hakuna mrejesho wa mara kwa mara unaoeleza ni kiasi gani kimetumika na kimeleta matokeo gani. Alisema kuwepo kwa mfumo wa kitaifa wa uwajibikaji utasaidia kuondoa sintofahamu na kujenga imani kwa wananchi.

Uchambuzi wa jamii: Ushahidi wa athari za mabadiliko ya tabianchi nchini

Ripoti za tathmini za hatari za mabadiliko ya tabianchi zinaonyesha kuwa takriban asilimia 70 ya majanga yanayohusiana na hali ya hewa nchini Tanzania yanachangiwa na mabadiliko ya tabianchi, hali inayoweza kusababisha hasara inayokadiriwa kufikia karibu asilimia 2 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa uchambuzi wa Climate Action Network Tanzania (CAN Tanzania).

Ripoti hizo pia zinaeleza kuwa kuongezeka kwa mvua zisizoeleweka, vimbunga pamoja na vipindi virefu vya ukame vinavyoathiri uzalishaji wa kilimo, hasa kwa wakulima wadogo, ni miongoni mwa athari zinazoongezeka kwa kasi kutokana na hali ya hewa isiyotabirika, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya kukabiliana na hatari hizo.

Hii inathibitisha kuwa pamoja na fedha zilizopo, bado Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa za athari za tabianchi, ikihitaji ufuatiliaji unaoonyesha ni miradi gani inaboresha ustahimilivu wa jamii.

Hitimisho

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania imeanza kupata fedha muhimu kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini ukosefu wa mifumo ya uwazi na ufuatiliaji unaelezwa na wataalamu kuwa kikwazo kikubwa. Ushahidi wa kisayansi unaonyesha athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wananchi wengi na umuhimu wa mifumo ya tathmini ya athari ili kuhakikisha ahadi za COP zinakuwa na matokeo halisi.

Kwa hivyo, wataalamu na watazamaji wa sera wanapendekeza mfumo wa kitaifa wa uwajibikaji unaoingiza takwimu za fedha, tathmini ya athari, na ushiriki wa wananchi ili kuhakikisha ahadi za COP zinakua za kweli na zinaimarisha ustahimilivu wa jamii.