Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kuwa uamuzi wa kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulikuwa wa hekima na busara, kwani haki haiwezi kupiganiwa nje ya uwanja wa mapambano ya kidemokrasia.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Othman Masoud Othman, wakati akizungumza na wanachama kuhusu hatua zilizofikiwa katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kisiasa kufuatia changamoto zilizojitokeza kwenye uchaguzi mkuu.
Amesema kushiriki uchaguzi uliopita kuliipa chama fursa ya kutambua mapungufu, ubadhirifu na kasoro zilizopo katika mfumo wa uchaguzi, jambo lililowezesha kuingia kwenye mazungumzo ya kutafuta maridhiano.
“Huwezi kupigania haki ukiwa nje ya mapambano. Kushiriki kwetu kulituwezesha kuonesha dunia kasoro zilizopo katika chaguzi za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema Othman.

Amesisitiza kuwa kususia uchaguzi hakuwezi kuwa suluhisho, kwani kungekosesha ushahidi wa kuonesha changamoto zilizopo katika sheria na mifumo ya uchaguzi.
Aidha, aliwataka wanachama kuendeleza umoja na mshikamano ili kufanikisha malengo ya chama, akieleza kuwa ushiriki wao kwenye uchaguzi uliowezesha hata kuwasilisha malalamiko rasmi kuhusu kasoro za uchaguzi.

Mapema, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, amesema mshikamano wa wanachama ndio uliofanya chama hicho kuendelea kupata heshima kubwa nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti mstaafu, Juma Duni Haji, amesema anajivunia kushiriki katika juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu kwa ajili ya umoja wa Wazanzibari wa sasa na vizazi vijavyo.

Aliwashukuru kwa moyo wa heshima DK Muhammed Ali Sheni na Dk Aman Abeid karume kwa busara na mchango wao wakiweka maslahi mapama ya nchi katika kutafuta suluhu ya kudumu visiwani Zanzibar
“Pia nisiwache kuwapongeza nyinyi wanachama wenzangu kwa ustahamilivu mlionyesha tukaeni mkao wa kula” ameongeza Duni.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Omar Ali Shehe, amewataka wanachama kuwaunga mkono viongozi wao katika juhudi zinazoendelea za kutafuta suluhu ya kisiasa Zanzibar.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani