March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pengo ufutiliaji fedha za tabianchi linavyoathiri uwajibikaji wa ahadi za COP Tanzania

Na Martha Fatael,Timesmajiraonline

WAKATI Tanzania ikiendelea kuwasilisha mafanikio yake katika majukwaa ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi, wataalamu wa mazingira na sera za tabianchi wanaonya kuwa bado kuna pengo kubwa la uwajibikaji, hususan katika ufuatiliaji wa fedha za tabianchi na tathmini ya athari za miradi inayotekelezwa.

Mtaalamu wa sera za tabianchi kutoka Climate Action Network Tanzania (CAN Tanzania), Boniventure Mchomvu, anasema moja ya viashiria muhimu vinavyokosekana katika utekelezaji wa ahadi za COP nchini ni kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kufuatilia fedha za tabianchi.

“Moja ya kipimo muhimu kabisa kinachokosekana Tanzania ni mfumo wa kufuatilia fedha za tabianchi. Kwa sasa tunadocument zaidi miradi iliyopita serikalini, lakini ile inayotekelezwa na wadau wengine wengi haionekani kabisa kwenye mfumo wa ufuatiliaji,” anafafanua Mchomvu.

Kwa mujibu wake, hali hiyo inasababisha serikali na wadau kushindwa kupata picha kamili ya kiasi cha fedha kinachoingia kwenye sekta ya tabianchi, miradi inayotekelezwa, na iwapo fedha hizo zinaisaidia jamii kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Miradi inatekelezwa lakini athari hazipimwi

Mchomvu anaongeza kuwa kipimo kingine muhimu cha uwajibikaji ni jinsi miradi inavyotekelezwa na jinsi inavyoathiri jamii, hasa katika kuimarisha uwezo wa kustahimili changamoto.

“Hatupaswi kuishia kuorodhesha miradi iliyotekelezwa… kiashiria kikubwa ni miradi ipi imetekelezwa na imeleta athari gani katika kujenga ustahimilivu wa jamii,” anasema.

Kauli hiyo inaibua maswali mapya kuhusu namna Tanzania inavyopima mafanikio ya ahadi zake za COP, hasa kwa jamii za vijijini zinazokumbwa na ukame, mafuriko, na mabadiliko ya mifumo ya mvua.

Maoni ya wananchi

Mkazi wa Kijiji cha Maji Moto wilayani Hai, Glory Manase, anasema
“Miradi mingi inafanyika hapa lakini tunashindwa kuona tofauti. Tunahitaji taarifa wazi za jinsi fedha zinavyotumika na athari zake kwa maisha yetu.”

Mkazi wa Kijiji cha Machame, Haruna Nyoni, anasema
“Tunashukuru miradi inapoletwa hapa, lakini mara nyingi tunasikia tu kuhusu ripoti za miradi, siyo matokeo halisi. Tunaona kama tunakosa sehemu yetu ya taarifa.”

Mkazi wa Himo, Amina Salum anatoa maoni
“Wakati ukame ukitokea, miradi ya kuweka mifumo ya maji haionekani kutusaidia moja kwa moja. Tunahitaji mifumo ya uwazi, ili tuweze kuona ni kiasi gani kinachotumika na ni faida gani kwa kila kijiji.”

Mapendekezo ya wataalamu ndani na baada ya COP

Katika mkutano wa COP29 uliofanyika Baku, Azerbaijan, wataalamu kadhaa wa Afrika waliisisitiza haja ya nchi zinazoendelea kuweka mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za tabianchi.

Akizungumza katika kikao cha pembeni (side event) kuhusu uwajibikaji wa fedha za tabianchi, Dkt. Richard Muyungi, Mjumbe wa Kikosi cha Majadiliano cha Afrika (AGN) na Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, alisisitiza umuhimu wa kuunganisha taarifa za kifedha na athari halisi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Dkt. Fatima Denton, Mkurugenzi wa UNU Institute for Natural Resources in Africa (UNU-INRA), aliyetoa mada katika jukwaa la wataalamu wa Afrika baada ya COP, alieleza kuwa nchi nyingi zinakosa mifumo ya kupima kama miradi ya tabianchi inaboresha maisha ya wananchi au inabaki kwenye ripoti pekee.

Nchini Tanzania, hoja kama hizo zimeendelea kujitokeza hata baada ya COP. Akizungumza katika mjadala wa sera za tabianchi ulioandaliwa Dar es Salaam na mashirika ya kiraia mwishoni mwa 2025, Profesa Patrick Luganda, mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisisitiza kuwa uwajibikaji wa ahadi za COP hauwezi kupimwa bila kuhusisha jamii na kuweka mifumo ya wazi ya taarifa.

Uwajibikaji unaanzia chini

Wataalamu hawa wanakubaliana kwamba bila mfumo wa kitaifa wa kufuatilia fedha za tabianchi, kutathmini athari za miradi, na kushirikisha wadau wote, Tanzania itaendelea kuonekana imetekeleza ahadi zake kimataifa, huku athari halisi kwa wananchi zikibaki kuwa hafifu.

Kwa mtazamo huu, mjadala wa uwajibikaji baada ya COP haupaswi kuishia kwenye sera na mikutano ya kimataifa pekee, bali uanze chini kwa kuweka mifumo ya uwazi, tathmini ya athari, na ushiriki wa jamii kama nguzo kuu za utekelezaji wa ahadi za tabianchi.