Na Irene Clemence, TimesMajira Online
KAMATI ya Amani ya Viongozi wa dini Mkoa wa Dar es Salaam imewaomba viongozi wa dini nchini kuacha kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa kwani kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha amani ya nchi .
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum ambaye amesema kuwa, baadhi ya viongozi wa dini wameanza tabia ya kuwanadi wagombea katika nyumba za ibada jambo ambalo halitakiwi kufanyika na kupelekea kuvunja amani ya nchi.
Amesema, kitendo hicho kinachofanywa na baadhi ya viongozi wa dini kinaweza kupelekea kuvuruga amani iliyopo na kupelekea kuweka matabaka.
Sheikh Salum amesema, kazi kubwa ya viongozi wa dini ni kuhubiri amani na si kusimamam katika nyumba za ibada na kuaza kufanya kampeni kwani si jukwaa sahihi.
“Sisi kwa umoja wetu viongozi wa dini wote wa kamati za amani na kwa ujumla wake hatupendezwi na tabia iliyoanza kujitokeza kwa sasa ya kuona maaskofu, mashekhe, Mapadri maimamu wanasimama katika nyumba za ibada kufanya kampeni na kumnadi Mgombea yoyote kufanya hivi ni kuatarisha amani ya nchi yetu”amesema Sheikh Salumu
Amesisitiza kuwa, nyumba za ibada zikianza kufanya kampeni zitakuwa zimepola nafasi za wanasiasa na majukwaa yao.
“Kama unamuitaji na unampenda mtu na unaona anatosha toka madhabauni na nenda katika maeneo ambayo utaweza kumfanyia kampeni mgombea wako kwani kiongozi wa dini anapofanya hivyo anakuwa anawakosea waumini wake na kuwalazimisha mtizamo wa kwake binafsi na kuwadhurumu haki yao, ” amesema Sheikh Salumu
Amesema, watanzania wanapaswa kuachwa waende katika majukwaa ya siasa wakasikilize sera za wagombea ili waweze kuchagua ni nani anawatosha na kuwataka viongozi wa dini kutokutumiwa na wanasiasa kutumika kwa namna yoyote kwani nchi ya Tanzania inatagaza amani amani kwanza kwani uchaguzi utapita hivyo ni muhimu kuilinda amani iliyopo .
“Amani tunaanza kuivurunga viongozi wa dini kitu ambacho ni hatari sana. Amani waivurunge wanasiasa sisi tutegeneze ikianza kuvurugwa na sisi viongozi dini kwa kuanza kuwafanyia kampeni wagombea fulani kwa kuwataja hii inakuwa aileti sura nzuri na kuweza kutuharibia mustakabari na makubaliano ya viongozi wa dini”amesema Sheikh Salumu
Amesisitiza kuwa, viongozi wa dini kwa sasa wanajukumu la kuwaombea viongozi pamoja na nchi kwa ujumla ili uchaguzi uweze kumalizika kwa salama na amani.
“Nasisitiza kamwe tusikubali nyumba nzetu za ibada kutumika na kufanya kampeni za wagombea jambo hili alifai hata kidogo” amesema Sheikh Salumu
Aliongeza kuwa kamati za amani nchi nzima zimekubaliana kuwa nyumba za ibada zisiingiliwe na kutumika na wanasiasa na wala kuwasemea.
Makamu Mwenyekiti wa kamati za amani Mkoa wa Dar es Salaam George Fukwe kutoka kanisa la KKKT usharika wa Kariakoo amesema, nyumba za ibada zinapaswa kutumika kwa ajili ya ibada na Sara na si viginevyo
Amesema, kipindi hiki ni muhimu sana viongozi wa dini kufanya dua na sala kuliombea taifa katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
“Katika kipindi hiki tunapaswa kutoa mafundisho ya haki na amani kwamba haki itendeke na amani iendelee kuwepo kwa maana hiyo atupaswi kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa na badala yake tuelekeze watu kutenda haki” amesema Fukwe
Naye Mjumbe wa kamati hiyo Askofu Silvester Gamanywa ambaye pia ni kiongozi wa Taasisi ya Wapo Mission International amesema, wajibu wa viongozi wa dini katika kipindi hiki kuombea amani na kuepuka kuchochea hisia kwa Wananchi zinazoweza kuvuruga amani ya nchi .
Katika mkutano huo pia umehudhuriwa na Wajumbe Wa kamati ya amani ikiwemo Maaskofu, manabii, wachungaji, Maimamu na Masheikh.
More Stories
Nani kuwa mrithi wa Kinana CCM?
Watendaji Songwe wapatiwa mafunzo uboreshaji daftari la mpiga kura
Samia: Mwaka 2024 ulikuwa wa mafanikio