March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA:Mvua za wastani hadi juu ya wastani kunyesha msimu wa mvua za masika

Na Penina Malundo,Timesmajira

MAMLAKA ya hali ya hewa nchini (TMA)imetoa mwelekeo wa Mvua za Msimu wa Masika kwa Machi hadi Mei 2026 huku zikitabiri uwepo wa mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini pamoja na baadhi ya maeneo ya magharibi mwa ukanda wa Ziwa Viktoria.

Mvua hizo zinatarajiwa kuanza kunyesha wiki ya nne ya mwezi Februari na ya kwanza ya mwezi Machi,2026 katika maeneo ya kanda ya Ziwa Victoria huku wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi zinatarajia kunyesha katika maeneo ya pwani ya kaskazini, na wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi,2026 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki.

Akitoa mwelekeo wa mvua hizo za masika jana jijini Dar es Salaam,mbele ya waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa TMA,Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC),Dkt. Ladislaus Chang’a alisema mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei na wiki ya kwanza ya mwezi Juni 2026 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Amesema ongezeko la mvua hizo zinatarajiwa mwezi Aprili,2026.”Mwelekeo wa mvua uliotolewa umezingatia zaidi kipindi cha mvua za Masika (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa.Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi vitazingatiwa katika utabiri wa kila siku na utabiri wa kila mwezi.

”Watumiaji wa taarifa ya hali ya hewa wanashauriwa kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),”amesisitiza.

Aidha msimu wa mvua za Masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki Mikoa ya (Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mkoa wa Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Chang’a amesema kwa mvua za Masika zinazotarajiwa kuwa za Wastani hadi Juu ya Wastani katika baadhi ya maeneo ya magharibi mwa ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita) pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma. Aidha, mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari na wiki ya kwanza ya mwezi Machi na kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2026.

Amesema katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini,mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi na kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei na wiki ya kwanza ya mwezi Juni, 2026. huku kwa upande wa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki mvua zinatarajia kuwa za Wastani hadi Chini ya Wastani na zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi na kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei, 2026.

Dkt. Chang’a amesema TMA imeendelea kutoa ushauri
kwa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii,kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

Miongoni mwa sekta hizo ni pamoja na Kilimo na Usalama wa Chakula,Mifugo na Uvuvi,Utalii na Wanyamapori,Ujenzi,Usafiri na Usafirishaji,Nishati,Maji na Madini pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa,”amesema