Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA),imetakiwa kufanya kazi kwa karibu na sekrtarieti zote nchini na sekta binafsi ili kuwawezesha watanzania kuwekeza zaidi katika miradi yao binafsi na kwa njia ya ubia na wageni.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga,amezungumza hayo Februari 4,2026,wakati wa akifungua kongamano la uwekezaji Kanda ya Ziwa lililofanyika mkoani hapa,na kushirikisha mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga na Kagera,ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya uwekezaji kwa mwaka 2026 yenye kauli mbiu “Unawezeshwa kuwekeza kwa kupewa unafuu wa mtaji”.

Amesema,majukumu ya TISEZA ni kuratibu, kuhimiza, kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi na kuishauri Serikali kuhusu sera ya uwekezaji nchini hivyo ni wajibu kufanya kazi kwa ukaribu na sekrtarieti zote na sekta binafsi.
Pamoja na kuelezea mikakati iliyofikiwa na Serikali katika kusimamia suala la uwekezaji kwa kuanzisha madawati ya kutolea huduma za uwekezaji katika mikoa mbalimbali nchini hususani mikoa isiyokuwa na Ofisi za Kanda za TISEZA pia ameielekeza mamlaka hiyo,kutembelea mikoa yote 26 ya Tanzania ili kutoa elimu ya uwekezaji kwenye maeneo yao.
Kapinga amesema, hakuna nchi iliyokua kiuchumi duniani bila kuwezesha na kukuza watu wake kuweza kuhodhi sehemu kubwa ya uchumi wao kupitia uwekezaji na biashara.
Amesema mwaka 2025 TISEZA ilitekeleza kwa mara ya kwanza kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani na kufanikiwa kuongeza idadi ya miradi iliyosajiliwa kutoka miradi 901 mwaka 2024 na kufikia miradi 927,kati ya miradi hiyo inayomilikiwa na Watanzania ilikuwa 469 sawa na asilimia 51.
“Kampeni hii iwe endelevu na ifikie mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, ili watanzania waweze kuelewa dhana ya uwekezaji na kupata taarifa muhimu za uwekezaji na hatimaye kusajili miradi na kunufaika na vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi vinavotolewa na Serikali kupitia vyeti vya uwekezaji na leseni,”amesema Kapinga.
Sanjari na hayo Kapinga amesema, uwekezaji nchini unalenga kutatua changamoto mbalimbali katika Jamii na kuleta ufanisi na faida mbalimbali zinazochangiza na kukuza uchumi wa nchi.
“Kuvutia mitaji ya wawekezaji kuleta teknolojia mpya na kisasa kwa watanzania pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana,”amesema Kapinga.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TISEZA,George Mkono,amesema kampeni ya mwaka huu ya kuhamasisha uwekezaji kwa watanzania kauli mbiu yake isemayo “Mtanzania awezeshwe kuwekeza kwa kupewa unafuu”.
Amesema,kauli mbiu hiyo imelenga kuwajengea Watanzania imani kwamba Serikali imeweka mazingira wezeshi,motisha na mifumo rafiki inayowezesha kuwekeza kihalali,kistarabu lakini kwa tija.
Pia amesema,kongamano hilo kwa Kanda ya Ziwa ni fursa adhimi Kwa ajili ya kutambua fursa za uwekezaji zilizopo katika eneo hilo ikiwa na rasilimali nyingi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo,biashara,uvuvi,viwanda,madini pamoja huduma nyingine.
“Lengo letu ni kuona fursa hizi zinatumika Kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wa Kanda ya Ziwa na taifa kwa ujumla,”amesema George.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema,Mkoa huo ni kitovu cha Mikoa ya Kanda ya Ziwa una fursa nyingi za uwekezaji ambazo zinajumuisha sekta ya kilimo,ufugaji,uvuvi wa kawaida na wa kisasa kwa njia ya vizimba,viwanda vya kuongeza thamani ya mazao,mifugo,samaki na madini pia utalii,ujenzi wa nyumba,kumbi za starehe na sinema pamoja na viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Pia amesema zipo fursa za uwekezaji katika maeneo ya usafiri na usafirishaji na huduma nyingine za kibiashara.
“Katika kuvutia uwekezaji Mkoa umetenga hekta 4,425 katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri zake kwa lengo la kuwekeza na kuendeleza maeneo hayo kwa shughuli mbalimbali.Tupo hatua nzuri sana wilayani Magu,kwa ajili ya ukanda wa viwanda na tayari Halmashauri inafanya vizuri na wawekezaji kadhaa wamejitokeza kuonesha nia ya kuanzisha viwanda vikubwa katika eneo hilo,”amesema Mtanda.
Mtanda amesema,Mkoa huo kwa sasa unapokea wafanyabiashara kutoka nchi za Kenya,Uganda,Burundi,Rwanda,Congo na Sudan huku akisisitiza kuwa imani yake kuwa wataendelea kuongezeka kutokana na kuimarika kwa miundombinu ikiwemo daraja la J.P.Magufuli.
“Utekelezaji wa kampeni hii katika Kanda Ziwa utaongeza kasi ya uwekezaji wa ndani na idadi ya wawekezaji hususani Mkoa wa Mwanza kwani Mikoa ya Kanda hii inachangia takribani asilimia 25 ya Pato la Taifa, hivyo miradi ya uwekezaji itakayotekelezwa itaongeza zaidi mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa,”amesema Mtanda.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina