March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gulamali ahoji mpango wa serikali kuboresha huduma za mawasiliano

MBUNGE wa Jimbo la Ilongelo, Hidary Gulamali, amehoji Bungeni kuhusu mpango wa Serikali wa kuboresha huduma za mawasiliano kwa kujenga minara katika maeneo ya jimbo lake yanayokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mtandao na mawasiliano ya simu.

Akiuliza swali la nyongeza wakati wa kikao cha Bunge kilichofanyika jijini Dodoma, Gulamali alieleza kuwa changamoto ya mawasiliano imekuwa kikwazo kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya jimbo lake, hususan katika shughuli za kiuchumi, kielimu na kijamii.

Mbunge huyo alitaja kata za Namuhunga na Ilongelo kuwa miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto kubwa ya mawasiliano, hali inayowalazimu wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za simu na mtandao.

“Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya mawasiliano katika kata za Namuhunga na Ilongelo zilizopo Jimbo la Ilongelo?” alihoji Gulamali mbele ya Bunge.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, alisema Serikali imetambua changamoto ya mawasiliano inayokabili maeneo mbalimbali nchini, hasa vijijini, na imechukua hatua za makusudi kuikabili.

Alisema Serikali imeandaa mkakati mahsusi wa miaka mitano unaolenga kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo yote yenye changamoto ya huduma hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za uhakika.

Dkt. Mkama alimhakikishia mbunge huyo kuwa kata za Namuhunga na Ilongelo pamoja na maeneo mengine yenye changamoto katika Jimbo la Singida Vijijini zitafikiwa kupitia utekelezaji wa mkakati huo wa Serikali.