March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Kitila kuwasilisha Bungeni kesho Mpango wa maandalizi kuanza kwa utekelezaji wa Dira 2050

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

KATIBU Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango(NPC),Dkt. Fred Msemwa ametoa wito kwa wananchi na wadau wote kufuatilia uwasilishaji wa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu 2026/2027-2050/2051), Mpango wa Nne wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2026/2027-2030/2031) na mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/2027.

Amesema mpango huo utawasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma 2 Februari 2,2026 na Serikali kupitia Waziri wa Nchi  Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo.

Dkt.Msemwa ametoa wito huo jijini hapa leo,Februari Mosi,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu maendeleo ya maandalizi ya kuanza Utekelezaji wa Dira 2050 ambao utaanza rasmi Julai Mosi ,2026.

“Kama mnavyofahamu,Tarehe 17 Julai 2025 Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua DIRA 2050 na Serikali kupitia NPC imeendelea na maandalizi ya NYEZO KUU TATU zitakazowezesha kuanza utekelezaji wa Dira 2050,@amesema.

Dkt.Msemwa amesema kuwa Mipango hiyo imepitia ngazi zote za uamuzi Serikalini na kesho, siku ya Jumatatu Tarehe 2 Februari 2026, Mipango hiyo itawasilishwa huku atoa msisitizo  wa kwanini Wananchi wanatakiwa kufuatilia kwa uzito mkubwa hatua iliuofikiwa katika Maandalizi ya Utekelezaji wa Dira 2050, wakati mipango hiyo mitatu ikiwasilishwa bungeni na kujadiliwa kwa wiki nzima.

Ambapo ametaja sababu kuwa  Dira hiyo ya  2050 imebeba matumaini ya Watanzania na imeandikwa kwa kuzingatia maoni yao. Hivyo basi, ni muhimu kwa wananchi kujua na kufuatilia mipango iliyoandaliwa ili kutekeleza Dira yao.

“Ni fursa ya kipekee kwa kila mwananchi kwani uwasilishaji wa Mipango hii mitatu itakayotekeleza Dira 2050 ni jambo lisilotokea mara kwa mara kwani utatokea tena baada ya miaka 25 ijayo. Hivyo ni muhimu kwa sisi wananchi tukafuatilia mustakabali wa Taifa letu,”amesema

Vilevile amesema Dira hiyo 2050 inasisitiza kuhusu ustawi wa pamoja na ushiriki wa kila mmoja wetu katika ujenzi wa Taifa letu. Dira 2050 ni alama ya Umoja wetu na nia thabiti ya kutomuacha nyuma Mtanzania hata mmoja. Hivyo basi ni muhimu kwa kila Mtanzania kuwa na taarifa kamili ya kinachoendelea katika Mipango ya Maendeleo ya Taifa letu.