Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameridhia tena kibali cha Ajira ya Watumishi 41,500 za watumishi wa Kada mbalimbali kama vile watumishi wa Kada za Afya, Walimu, Kilimo, Afya, Uvuvi, Wahandisi, Zimamoto na Uokoaji, Uhamiaji, Magereza, Jeshi la Polisi na watumishi wa kada mbalimbali.
Ridhiwani amesema hayo jijini hapa leo Januari 30,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekeleza wa ahadi za Rais Samia katika kipindi chake cha pili.
Amesema katika kutekeleza Maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,Serikali imetoa kibali cha ajira Kwa nafasi 12,000 za ajira zikiwemo nafasi 5,000 za kada za Afya na nafasi 7,000 za Walimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati ikiwa ni Sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya sita.
Ambapo amesema hadi sasa jumla ya watumishi 8,416 wameripoti katika halmashauri mbalimbali nchini, wakiwemo watumishi 3,694 wa kada ya elimu na watumishi 4,722 wa kada ya afya.
“Baada ya ajira hizi Rais Samia katika siku 100 zake ameridhia tena kibali cha ajira ya watumishi 41,500 hivyo naendelea kutoa rai kwa Watanzania wenye sifa kuendelea kujitokeza kwa wingi kuomba ajira katika Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma watapotangaza nafasi mbalimbali za ajira,”amesema.
Aidha amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa nafasi ya ajira na kuzitangaza ambapo imewataka vijana wote wenye sifa waendelee kuomba nafasi mbalimbali kwa kadri zitakapotangazwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Pamoja na hayo Waziri huyo amesema kutokana na kuwepo kwa maombi mengi ya kubadilisha vituo vya kazi ametoa rai kuwa hakutakuwa na mabadiliko ya vituo vya kazi kwakuwa nafasi hizi za ajira zimetolewa kulingana na uhitaji wa kila Halmashauri au mwajiri husika.
“ Hivyo, kubadili kituo maana yake ni kupunguza idadi ya watumishi waliopangwa kwenda Halmashauri husika. Ili kutoathiri ugawaji wa nafasi hizi, hakuna mabadiliko yoyote ya vituo yatakayofanyika,”amesema.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani