*Yaelekeza asilimia 60 ya mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela ilielekeza asilimia 60 ya fedha zilizokusanywa katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/26 katika utekekalezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ambapo Halmashauri hiyo katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/26,imekusanya zaidi ya bilioni 7 sawa na asilimia 42.9 ya makisio ya mapato ya ndani ya bilioni 16.45.

Hayo yamebainishwa Januari 29,2026 na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Dkt. Maria Kapinga,wakati akiwasilisha taarifa katika mkutano wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za utekekalezaji robo ya pili kipindi cha Oktoba-Desemba 2025/26.
Ambapo amesema kati ya fedha zilizokusanywa asilimia 60 zilielekezwa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zaidi katika sekta za elimu na afya.
Amesema,kwenye elimu zilielekezwa katika ununuzi wa madawati na ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Huku katika sekta ya afya zikielekezwa kwenye ujenzi wa zahanati za Nyambiti na Nyafula pamoja na kuboresha huduma za upasuaji katika kituo cha afya Kayenze.
Dkt.Kapinga,amesema halmashauri hiyo imeendelea kutenga asilimia 10 ya mapato yasiyofungwa kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hadi sasa jumla ya milioni 625 zimekopeshwa kwa vikundi mbalimbali.
Sanjari na hayo amesema, katika kipindi hicho Halmashauri hiyo imetekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya bilioni 43.9 kupitia mapato ya ndani, ruzuku ya Serikali Kuu pamoja na fedha za Mpango wa Uendelezaji Miji na Majiji (UCDG).
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Sarah Ngh’wani,amewataka madiwani, wataalamu na wananchi kudumisha amani na mshikamano ili kuiendesha halmashauri kwa ufanisi.
Ambapo amesema, ipo haja ya kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kufikia malengo ya maendeleo na ustawi wa wananchi wa Ilemela huku akiwasisitiza wataalamu kujikita katika majukumu yao ya msingi.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Mariamu Msengi,amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo unahitaji fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani, hivyo ushiriki wa wataalamu katika ukusanyaji wa mapato ni muhimu ili miradi itekelezwe kwa ubora na kuwanufaisha wananchi.

Hata hivyo,Diwani wa Kata ya Buzuruga,Manusura Sadick,amesema wananchi wanahitaji maendeleo kwa vitendo badala ya maneno huku akisisitiza kuwa haiwezekani kutekeleza miradi bila fedha hivyo amewahimiza wataalamu kuongeza kasi ya ukusanyaji katika miezi mitano iliyobaki ya mwaka wa fedha.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi