March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANFORD yaandaa Kongamano Dubai la wafanyabiashara

Na Penina Malundo,Timesmajira

Umoja wa Wawakilishi wa Mawakala wa Usafirishaji wa Mizigo wa Tanzania waliopo Dubai ujulikanao kama Tanzania Freight Forwarders Representation in Dubai (TANFORD) umeandaa kongamano katika Umoja wa Nchi za Kiarabu, Dubai lengo likiwa ni kuinadi Tanzania katika masoko ya kimataifa na kufungua fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.

Kongamano hilo linalotarajia kufanyika siku mbili katika umoja huo na kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kufungua fursa za kibiashara.

Akizungumza na waandishi wa Habari jana Jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa TANFORD,Hussein Jamal amesema kuwa kongamano hilo linaloitwa Tanzania Trade and Logistics Forum 2026 litafanyika kati ya Februari 13 na 14 mwaka huu kuwakunisha wadau mbalimbali wa sekta ya biashara na usafirishaji.

Amesema kongamano hilo linalengo la kufungua fursa zilizopo baina ya Tanzania na Dubai katika sekta ya uwekezaji na biashara .

“Tumeandaa kongamano hili ili kuinadi nchi yetu kimataifa na kuifanya nchi yetu kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji afrika mashariki na kati na pia kusaidia kukuza matumizi ya bandari na miundombinu ya usafirishaji Tanzania kwa kukusanya mizigo katika masoko ya kimataifa kupita Tanzania,” amesema Jamal

Jamal amesema kuwa kongamano hilo litasaidia kufungua fursa za masoko mapya ya bidhaa za kitanzania kuweza kufika kimataifa kwa kukutana na wateja mbalimbali ambao wanatarajiwa kuwepo kwenye kongamano hilo.

”TANFORD inasimama kama Daraja la kibiashara katai ya Tanzania na masoko ya kimataifa ili kuweza kuwasaidia watanzania wengi kuweza kuona fursa mbalimbali za biashara na usafirishaji zilizopo Dubai na pia kutangaza biashara zao huko,”amesema

Aidha amesema ni fursa adhimu kwa wadau mbalimbali katika kushiriki kongamano hilo hivyo wameweza kuwakaribisha wadau wengine kushiriki kwa lengo lakwenda kufungua fursa kwa mtu mmoja mmoja, kwa taifa na makampuni yanayofanya biashara ya usafirishaji kati ya Dubai na Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt Latifa Mohammed Khamis amesema kuwa ni muhimu kushiriki katika makongamano kama hayo kwani husaidia kukuza mahusiano bora baina ya wafanyabiashara wa hapa nchini na wa nje ya nchi.

“Rai yangu kwa wafanyabishara wa kitanzania ni muhimu kuudhuria kongamano hili kwani litafungua fursa ya kupata mashirikiano mbalimbali na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali,”ameleza.

Naye rais wa Chama cha Mawakala forodha Tanzania (TAFFA),Edwin Urio amebainisha kuwa kushiriki katika kongamano hilo ni fursa ya kujikuza kibiashara, kujitagaza inakwenda kusaidia kukuza Uchumi wa Nchi.

“Sekta ya logistics na usafirishaji ndio sekta ambayo katika mwaka wa fedha uliopita 2024/2025 iliongoza katika kuingizia fedha za kigeni nchini na pia ni sekta ambayo ni uti wa mgongo wa Nchi yeyote ambayo inakua kiuchumi,”amesema Urio.

Miongoni mwa Taasisi tofauti zinazotarajia kushiriki katika Kongamano hilo ni pamoja na TPA, TRA, DP WORLD, TAFFA, TANTRADE, TATOA, PORT MARINE CLEARING & FORWARDING, SILENT OCEAN & KILIMANJARO STAR CARGO na TPSF.