March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yapaswa kuchukua hatua za uwajibikaji kutimiza ahadi za tabianchi

Na Martha Fatael, TimesMajiraOnline

MIAKA miwili baada ya Tanzania kutoa ahadi nzito katika mikutano ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na COP29 na COP30 maeneo mengi ya milimani nchini bado yanakabiliwa na athari zilezile za mabadiliko ya tabianchi bila kinga madhubuti.

Wakati viongozi wa taifa wakipaza sauti zao katika majukwaa ya dunia wakiahidi ulinzi wa milima na suluhu endelevu, utekelezaji wa ahadi hizo bado haujaonekana kwa kiwango kinachogusa maisha ya wakulima, wanawake na vijana wanaotegemea rasilimali za milimani kwa maisha yao ya kila siku. Kauli za kuanzishwa kwa mifumo kama Mfuko wa Kitaifa wa Tabianchi na Jukwaa la Suluhu za Milimani, pamoja na ahadi ya kuwasilisha Mpango wa Kitaifa wa Tabianchi baada ya COP30, zimeendelea kutolewa hadharani, lakini swali kuu linabaki ni nani anayewajibika kuhakikisha ahadi hizi zinabadilika kutoka maneno hadi vitendo vinavyoonekana kwenye ardhi ya watanzania wa milimani?

Ahadi za COP29: Milima kama kipaumbele cha kitaifa

Katika mkutano wa COP29, Tanzania ilijiunga na mataifa mengine kutambua mchango wa maeneo ya milimani katika usalama wa maji, chakula na ikolojia. Kupitia ujumbe wake rasmi, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa kuimarisha sera za ulinzi wa milima na kuongeza juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii zinazoishi maeneo hayo.

Akizungumza kuhusu mwelekeo wa Tanzania katika majadiliano ya tabianchi, Mjumbe wa Kikosi cha Majadiliano cha Afrika (African Group of Negotiators, AGN), Dkt. Richard Mayungi, alinukuliwa akieleza kuwa nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania, zinahitaji mifumo madhubuti ya ndani ili ahadi za kimataifa ziweze kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi. Alisisitiza kuwa bila utekelezaji wa kitaifa, maazimio ya COP yanabaki kuwa kauli za kisiasa.

Uhalisia wa miaka miwili baadaye

Licha ya msisitizo huo, uchunguzi unaonesha kuwa hadi sasa hakuna mifumo mahsusi iliyowekwa hadharani kuonesha utekelezaji wa moja kwa moja wa ahadi za COP29 kuhusu milima. Hakuna taarifa rasmi zinazoonesha, miradi mipya ya kitaifa inayolenga mahsusi maeneo ya milimani kufuatia COP29, Bajeti iliyotengwa moja kwa moja kwa utekelezaji wa ahadi hizo na Mfumo wa uwazi wa kufuatilia maendeleo ya ahadi za COP29

Hali hii inaacha pengo kati ya ahadi zilizotolewa kimataifa na hali halisi ya utekelezaji ndani ya nchi.

Serikali yasema iko kwenye mchakato

Katika mkutano wa COP30 na maelezo ya baada ya mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo, alinukuliwa akisema kuwa Tanzania imejizatiti kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuchukua hatua za kimkakati na kuimarisha uratibu wa kitaifa. Alieleza kuwa serikali inaendelea kuandaa mifumo ya ndani itakayosaidia kuratibu fedha na miradi ya tabianchi.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna ratiba ya wazi iliyotolewa hadharani inayoonesha ni lini mifumo kama Mfuko wa Kitaifa wa Tabianchi (ANCCF) au Jukwaa la Kitaifa la Suluhu za Milimani itaanza kufanya kazi kikamilifu.

Sauti za wananchi wa milimani

Kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya milimani kama Kilimanjaro, Rungwe na Lushoto, ahadi hizo bado hazijatafsiriwa katika maisha yao ya kila siku. Wakulima wanaripoti mvua zisizotabirika, mmomonyoko wa udongo na upungufu wa maji, hali inayozidi kuhatarisha uzalishaji wa chakula na kipato cha kaya.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, Anna Kiwango na Ado George wanasema bado hawajaona juhudi za moja kwa moja za wao kushirikishwaama kusaidiwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kama ahadi ahadi zinavyotolewa kwenye majukwaa na mikutano ya kimataifa.

“Wanawake na vijana, ambao ndio nguvu kazi ya shughuli nyingi za kilimo na uhifadhi, wameendelea kubeba mzigo mkubwa wa athari za tabianchi bila mifumo thabiti ya msaada wa kitaifa”anasema George.

Mtazamo wa Asasi za Kiraia

Akizungumzia pengo hilo, Mwakilishi wa Mashirika ya Kiraia katika masuala ya tabianchi, Fatma Khamis, alinukuliwa akisema kuwa changamoto kubwa si ukosefu wa ahadi bali ni utekelezaji wake. Alieleza kuwa bila mifumo ya uwajibikaji na uwazi, jamii za milimani zitaendelea kuathirika licha ya Tanzania kuonekana mstari wa mbele kwenye majukwaa ya kimataifa.

Uwajibikaji wa Taasisi

Kwa mujibu wa muundo wa serikali, utekelezaji wa ahadi za COP29 unapaswa kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kushirikiana na wizara za kisekta pamoja na Bunge kupitia usimamizi wa sera na bajeti. Hata hivyo, ukosefu wa taarifa za wazi kwa umma unafanya iwe vigumu kupima kiwango cha utekelezaji na kuwawajibisha wahusika.

Macho COP31

Kadri Tanzania inavyoelekea COP31, wadau wanahoji kama safari hiyo italeta ahadi mpya au mrejesho wa utekelezaji wa ahadi za awali. Kwa wananchi wa milimani, thamani ya ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya COP itapimwa kwa hatua zitakazochukuliwa nyumbani sio kwa hotuba, bali kwa vitendo vinavyoonekana.