March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA yajidhatiti shida ya maji Mji wa Lushoto kuwa historia

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) amewahakikishia Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuwa shida ya maji kwenye Mji wa Lushoto itabaki historia baada ya utekelezaji wa mradi wa maji kwenye mji huo kufikia asilimia 88.

Akizungumza Januari 24, 2026 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri hiyo robo ya pili, mwakilishi wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto, Fredy Mbulumi alisema mchakato wa kumlipa Mkandarasi awamu ya tatu wa sh. milioni 360 unaendelea ngazi ya mkoa.

“Tenki la Maji Mradi wa Lushoto mjini lililopo Magamba likiwa kwenye hatua za mwisho za ujenzi. Lina uwezo wa kuhifadhi lita 650,000.”

“Ujenzi wa Mradi wa Maji Lushoto Mjini unaojengwa kwa gharama ya sh. 1,800,919,263, huku kiasi kilicholipwa kikiwa ni sh. 965,034,663 kwa fedha za Mfuko wa Maji (NWF), na unaotekelezwa na Mkandarasi M/s PNR Services Ltd umefikia asilimia 88, na Mkandarasi anadai malipo ya awamu ya tatu (IPC NO.3) ya sh. milioni 360.3.

“Mchakato wa malipo hayo unafanyika mkoani ili aweze kuendelea na kazi, lakini baada ya malipo hayo, hatalipwa tena mpaka hapo atakapokamilisha mradi. Niwahakikishie madiwani, mradi huu unakwenda kukamilika na kuondoa changamoto zote za maji kwa wananchi wa Mji wa Lushoto na viunga vyake, na kuweza kupata maji ya uhakika” alisema Mbulumi.

“Mwakilishi wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto, Fredy Mbulumi.”

Mbulumi alisema pia wapo kwenye ujenzi wa Mradi wa Maji Mkundiambaru na Mkundiamtae wenye gharama ya sh. 787,204,963, na kiasi kilicholipwa ni sh. 507,594,693, na fedha zake zinatokana na Lipa kwa Matokeo (P4R), na Mkandarasi ni Buzunona & Sons Company Ltd. Mradi huo unaojengwa kwenye vijiji viwili vya Mkundiambaru na Mkundiamtae, ujenzi wake umefikia asilimia 99.

Mradi mwingine ni ukarabati wa Mradi wa Maji Gologolo/Hemtoye. Mradi huo ambao unatekelezwa kwenye kata mbili za Shume na Hemtoye kwa gharama ya sh. 1,353,414,436, na kiasi kilicholipwa ni sh. 257,219,822 kupitia NWF, ukiwa chini ya Mkandarasi N&J Investment Ltd, na umefikia asilimia 50 na Mkandarasi yupo kazini.

Awali, Ramadhan Ally ambaye ni
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, aliwaeleza Madiwani na Wakuu wa Idara kuwa suala la ukusanyaji mapato ni la kufa na kupona, kwani halmashauri inatakiwa iunde timu ya ukusanyaji mapato na iwe na uongozi wake kuanzia Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina.

“Madiwani wa Lushoto DC.”

Akifunga Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Whitney Mwizagi ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo tangu kuanzishwa kwa halmashauri hiyo, alisema anataka ushirikiano kati ya Madiwani na Wakuu wa Idara ili kuona halmashauri hiyo inapata ufanisi ikiwemo ukusanyaji mapato.

“Wakuu wa Idara, Vitengo, Maofisa Tarafa na vyama vya siasa wakiwa kwenye Baraza.”
“Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Whitney Mwizagi alipofungua Baraza.”
“Ramadhan Ally ambaye ni Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Tanga.”
“Tenki la Mradi wa Maji Mkundiamtae na Mkundiambaru lenye ujazo wa lita 90,000.”
“Tenki la lita 50,000 ambalo lipo upande wa Kijiji cha Mkundiambaru, Mradi wa Maji Mkundiambaru/Mkundiamtae.”